Na mwandishi wetu, Gazetini
NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema Mradi wa Umeme wa Jua unaotekelezwa Kishapu, mkoani Shinyanga, uko katika hatua za mwisho za ukamilishaji, ambapo jumla ya megawati 50 zinatarajiwa kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa ili kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani.
Salome ameyasema hayo Januari 9, 2026, wakati wa ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya umeme mkoani humo, ikiwemo Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu, Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli, pamoja na Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli hadi Mkoa wa Simiyu.
Amesema hadi sasa Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu umefikia zaidi ya asilimia 89 ya utekelezaji, na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu, hatua ambayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo endelevu.
“Mradi huu umefikia zaidi ya asilimia 89 ya utekelezaji wake, na tunatarajia kwamba ifikapo mwishoni mwa mwezi huu tutaingiza megawati 50 kwenye Gridi ya Taifa. Huu ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha pamoja na mtandao imara wa kusafirisha na kusambaza umeme,” alisisitiza Salome.

Akizungumza kuhusu Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli, ambao umefikia asilimia 44.32, Naibu Waziri huyo amesema mradi huo una umuhimu mkubwa kwa kuwa utawezesha kusambaza umeme kwenye reli ya kisasa ya SGR, pamoja na kupeleka umeme katika nchi jirani za Kenya na Uganda.
“Tunamshukuru na kumpongeza Mhe. Rais kwa kutoa fedha kwa ajili ya upanuzi wa Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli. Kwetu sisi ni heshima kubwa kwa kuwa kituo hiki kitahudumia mradi mkubwa wa kimkakati wa SGR, sambamba na kuimarisha usambazaji wa umeme katika nchi jirani,” alifafanua.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Miradi TANESCO, Mhandisi Frank Mashalo, amesema mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Ibadakuli hadi Simiyu unalenga kuimarisha upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Simiyu na mikoa jirani. Amesema hadi sasa mradi umefikia asilimia 53 na unatarajiwa kukamilika Juni mwaka huu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi, amesema kukamilika kwa Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu kutachochea shughuli za uzalishaji na kukuza uchumi wa wananchi wa eneo hilo, wengi wao wakijihusisha na kilimo cha pamba, ambacho kinahitaji umeme wa uhakika kwa ajili ya uzalishaji.
Mradi wa Umeme wa Jua Kishapu unatekelezwa kwa gharama ya sh bilioni 323 kwa awamu zote mbili. Mradi huo ulianza rasmi Desemba 2023 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Januari 2026.


