PARIS, Ufaransa
Mahakama ya Paris imewatia hatiani watu kumi kwa tuhuma za unyanyasaji wa mtandaoni dhidi ya mke wa Rais wa Ufaransa, Brigitte Macron, baada ya kusambaza madai ya uongo kwamba ni mwanamke aliyebadili jinsia baada ya kuzaliwa mwanaume, vyombo vya habari vya Ufaransa vimeripoti.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Brigitte Macron na mumewe, Rais Emmanuel Macron, wamekuwa wakilengwa mara kwa mara na madai ya kupotosha katika miaka ya hivi karibuni. Baadhi ya madai hayo yalidai kuwa Brigitte alizaliwa kwa jina la Jean-Michel Trogneux, ambalo kwa kweli ni jina la kaka yake mkubwa.
Licha ya wanandoa hao kuwa na tofauti ya umri wa miaka 24, madai hayo ya uongo yalipuuzwa kwa muda mrefu kabla ya kuanza kushughulikiwa rasmi kupitia mkondo wa kisheria.
Uamuzi wa mahakama umetolewa leo Jumatatu unaonekana kuwa faraja kwa wanandoa hao, hasa ikizingatiwa kuwa pia wanaendelea kufuatilia kesi nyingine maarufu ya kashfa nchini Marekani dhidi ya mtangazaji wa podikasti wa mrengo wa kulia, Candace Owens, ambaye pia amewahi kudai kuwa Brigitte Macron alizaliwa akiwa mwanaume.
Katika kesi ya Paris, wanaume wanane na wanawake wawili walipatikana na hatia ya kutoa maoni ya kashfa kuhusu jinsia ya Brigitte Macron, huku baadhi yao wakilinganisha tofauti ya umri wake na mumewe na kile walichokiita “unyanyasaji wa watoto.”
Mahakama imewahukumu kifungo cha hadi miezi minane jela, baadhi ya vifungo hivyo vikiwa vimeahirishwa, kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Ufaransa.


