MIAMI, Marekani
INTER Miami ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS) imeripotiwa kuwa mstari wa mbele katika kuiwania saini ya mpachikaji mabao wa Barcelona raia wa Poland, Robert Lewandowski.
Klabu hiyo anayocheza Lionel Messi, ambayo kocha ni Javier Mascherano, inamtaka Lewandowski ikiamini ataziba pengo la Luis Suarez anayetaka kuondoka mwishoni mwa msimu huu.
Huku mkataba wake ukitarajiwa kufikia ukomo Juni, mwakani, Lewandowski amekuwa kwenye kiwango bora msimu huu, akiwa amefunga mabao nane na ‘asisti’ mbili katika mechi 17.
Barcelona wanatajwa kutokuwa na mpango wa kumpa mkataba mpya straika huyo wa zamani wa Borussia Dortmund mwenye umri wa miaka 37.
Wakati huo huo, vigogo wa Serie A, AC Milan, nao wanaihangaikia saini yake, kama ilivyo kwa klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Saudi Arabia, kwa mujibu wa Gazeti la Marca la Hispania.


