WASHINGTON DC, Marekani
RAIS wa Marekani, Donald Trump, amemtaka mwenzake wa China, Xi Jinping, kumwachia huru mwanaharakati wa demokrasia mjini Hong Kong, Jimmy Lai.
Lai, ambaye pia ni mmoja ya mabilionea wakubwa barani Asia, anashutumiwa kwa kuhusika katika maandamano ya mwaka 2019 mjini Hong Kong.
Wakati huu Lai mwenye umri wa miaka 78 akiwa anasubiri hukumu ya kifungo cha maisha gerezani, Rais Trump ameibuka.
“Najisikia vibaya. Nilizungumza na Rais Xi kuhusu hilo na nilimuomba aangalie namna ya kumwachia,” amesema na kuongeza:
“(Lai) ni mzee kwa sasa na hata afya yake haiko sawa. Kwa hiyo, nimewasilisha ombi (kwa China). Ngoja tuone itakavyokuwa.”
Ni kwa maana hiyo, Trump anaungana na Serikali ya Uingereza, ambayo pia ilishatoa taarifa ya kutaka Lai kuachiwa mara moja.
Katika taarifa yake, Uingereza kupitia kwa Katibu wa Mambo ya Nje, Yvette Cooper, imesema mashitaka dhidi ya mfanyabiashara huyo ni ya kisiasa tu.
“Amekuwa akiandamwa na Serikali za China na Hong Kong kwa vile tu anatumia uhuru wake wa kujieleza,” amesema Cooper.
Lai, ambaye ni raia wa Uingereza, amekuwa chini ya ulinzi tangu alipokamatwa Desemba, 2020 na anatarajiwa kuhukumiwa mwanzoni mwa mwaka ujao.


