Na mwandishi wetu, Gazetini
Mabadiliko makubwa yanayoendelea ndani ya sekta ya nishati yanaanza kuibadili sura ya Jiji la Dar es Salaam, huku Serikali ikithibitisha kuwa miundombinu ya zamani haiwezi tena kukidhi kasi ya ukuaji wa watu, viwanda na huduma.
Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Desemba 11, 2025, baada ya Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, kutangaza kukamilika rasmi kwa mradi wa upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Kinyerezi 1 Extension, hatua inayojumuisha ufungaji wa Transfoma mpya ya kisasa yenye uwezo wa MVA 175.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika vituo vya uzalishaji umeme vya Kinyerezi I na II pamoja na Ubungo I, II na III, Mhe. Salome alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati mkubwa wa Serikali wa kulinda ustawi wa miji inayokua kwa kasi—hasa Dar es Salaam—kwa kuhakikisha umeme wa uhakika unakuwa msingi wa shughuli za biashara, viwanda, taasisi za huduma, na makazi yanayoendelea kupanuka.
Mbagala na Gongo la Mboto kupata nafuu ya muda mrefu
Maeneo ya Mbagala na Gongo la Mboto—miongoni mwa maeneo yenye makazi makubwa zaidi jijini—yamekuwa yakipata changamoto za kukatika kwa umeme kutokana na ongezeko kubwa la watu na majengo mapya.
Kwa kukamilika kwa mradi huu, Serikali inasema mzigo huo utaanza kupungua mara moja.
“Transfoma zimefungwa, majaribio yanaendelea, na mwezi huu wananchi wa Mbagala na Gongo la Mboto wataanza kuona tofauti,” amesema Salome.
Ameongeza kuwa hatua hiyo haihusu tu kuboresha huduma, bali pia kuandaa mazingira mpya unaoingia kwa kasi kusini mwa jiji.
TANESCO: Jiji limekua, miundombinu lazima ikue
Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, amesema Dar es Salaam imeongezeka kwa kiwango ambacho miundombinu ya miaka 10 iliyopita haiwezi tena kuhimili.
Amefafanua kuwa, Kinyerezi sasa ina Transfoma ya MVA 175, Gongo la Mboto na Mbagala zinawekewa Transfoma ya MVA 12, lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa usambazaji ili kufanya mzunguko wa umeme kuwa imara hata katika vipindi vya ongezeko la matumizi.

“Tunahakikisha umeme unaozalishwa Kinyerezi unawafikia wateja kwa kiwango kinacholingana na mahitaji ya sasa. Jiji limekua, na miundombinu lazima ikue,” amesema Twange.
Umeme wa uhakika kama injini ya uchumi mpya wa Dar es Salaam
Upanuzi wa Kinyerezi 1 Extension unatajwa kuwa sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuijenga Dar es Salaam kama kitovu cha uchumi wa ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa umeme wa uhakika: Viwanda vya kusindika na uzalishaji vinaweza kufanya kazi saa 24, huduma za afya, maji, mawasiliano na usafiri zinakuwa thabiti, wafanyabiashara wadogo na wa kati hupungua gharama za uendeshaji
Mradi huu unakuja wakati Serikali ikiendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya nishati ili kuhakikisha nchi inaingia kwenye zama mpya za uchumi unaotegemea viwanda na teknolojia.


