LILONGWE, Malawi
POLISI nchini Malawi wameanza uchunguzi juu ya tukio la mbwa wake wanne kupotea katika makazi ya rais mjini Lilongwe.
Ni katika uchunguzi huo, polisi wamekiri kupata kibali cha kupekua makazi ya rais wa zamani, Lazarus Chakwera, baada ya kupata taarifa kuwa mbwa hao aina ya ‘German Shepherds’ wamefichwa hapo.
Chakwera aliachia ofisi baada ya kubwagwa na Peter Mutharika katika kinyang’anyiro cha urais wakati wa Uchaguzi wa Septemba, mwaka huu.
Ikumbukwe, alishika nafasi ya pili akiwa na asilimia 33 ya kura na amekuwa akihusishwa na kashfa nyingi za ufisadi.
Awali, zilikuwepo taarifa kuwa Chakwera naye amekamatwa kwa tuhuma hizo, ingawa polisi wamekanusha.
Kwa upande mwingine, Godfrey Arthur Jalale, ambaye alikuwa mtumishi wa Ikulu wakati wa utawala wa Chakwera, anashikiliwa na polisi.
Arthur Jalale anashutumiwa kuhusika katika wizi wa mbwa hao, ingawa amekana mashitaka hayo.
Published:


