Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema yaliyotokea Oktoba 29, yameitia doa Tanzania na huenda yakaipunguzia sifa yakupata mikopo kwa urahisi na kuwataka mawaziri kujipanga kutafuta fedha kwa kutumia rasilimali za ndani.
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Novemba 18, 2025 katika hafla ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu Waziri iliyofanyika Ikulu Chamwino,jijini Dodoma. Ikumbukwe kuwa Oktoba 29 na 30, 2025 zilitokea vurugu za maandamano zilizosababisha vifo na uharibifu wa mali.
Akizungumza katika hafla hiyo amesema kuwa katika muhula wa kwanza wa awamu ya sita, Tanzania ilikuwa ikipata mikopo kwa urahisi kutokana na sifa, msimamo na kazi wanazofanya.
lakini kwa hali ilivyo sasa huenda nchi ikakosa kupata mikopo kwa masharti nafuu au kwa muda mfupi.

“Rasilimali zetu ni chache kama mnavyojua mara nyingi tunategemea kupata kutoka nje, mikpo kutoka taasisi mbalimbali za kimataifa, mabenki ya kimataifa, lakini yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo kwa hiyo huenda yakatupunguzia sifa za kupata hiyo mikopo kwa urahisi,” ameeleza Rais Samia.
Katika hatua nyingine amewasisitiza mawaziri hao kuwa wamepewa dhamana ya kuwatumiakia wananchi na haoni shida kubadilisha wanamjua.
“Majukumu tuliyopeana leo, dhamana tulizopeana leoni dhamana za kazi na si fahari kwamba na mimi ni waziri ikawa ndio fahari ulikotoka na unakokaa na kwingineko hapana, Tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi kauli mbiu yetu kazi na Utu tunasonga mbele na ule utu uanze na sisi wenyewe viongozi tunaokwenda kuwasimamia wengine,” amesisitiza.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika muhula wa kwanza wa Serikali ya awamu ya sita yametokana na mchango mkubwa wa mawaziri na viongozi aliokuwa akifanya nao kazi katika kipindi hicho.


