Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Rais Samia Suluhu Hassan amemuapisha Dk. Mwigulu Nchemba kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akimtaka kuhakikisha anaongeza kasi ya utendaji wa Serikali na kumtahadharisha na vishawishi vya ndugu na jamaa.
Hafla hiyo ya uapisho imefanyika leo Novemba 14,2025 Ikulu Chamwino, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu aliyemaliza muda wake, Kassim Majaliwa.
Akizungumza katika halfa hiyo, Rais Samia ameeleza kuwa utekelezaji wa kazi unahitaji fedha na kwamba Dk. Mwigulu ana uzoefu na anajua zilikokuwa zinapatikana, hivyo atamsaidia Waziri wa Fedha atakayeteuliwa kufanikisha hayo.


“Lakini utekelezaji wa kazi zote hizo zinahitaji fedha na wewe umetoka katika sekta ya fedha, kwa muda wa miaka mitano umejua vichochoro vyote tulivyokuwa tukipita kutafuta fedha. “Kwa hiyo utamsimamia atakayekaa kwenye nafasi yako (Wizara ya Fedha), ili naye aweze kupita kule tulikopita fedha ipatikane na kazi ifanyike. Kwa kifupi una kazi kubwa sana,” amesema.
Rais Samia amemwambia Dk. Mwigulu kuwa amepokea kijiti kutoka kwa Waziri Mkuu Mstaafu, Majaliwa ambaye alikuwa ni mfanyakazi mzuri aliyefanikisha mambo mengi, akiamini atafuata nyayo hizo na kuongeza juhudi sehemu zilizo na upungufu ili kuleta maendeleo zaidi nchini.
Akielezea mchakato wa kumpata Waziri huyo, amesema amepitia ushindani mkubwa na vigezo kadhaa, akiwashinda wenzake kwa sifa, mojawapo ikiwa ni uzoefu wa kuwatumikia wananchi kwa muda mrefu.


“Vigezo vyote vilivyopimwa, tumepima katika maeneo mbalimbali vya kuitumikia nchi hii na kulitumikia Taifa hili. Kubwa zaidi ni kuwatumikia wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema.
Aidha amemtaka kufahamu kuwa jukumu alilopewa ni zito na lina vishawishi anavyotakiwa kuepuka na badala yake ajielekeze zaidi katika kuwatumikia Watanzania.
“Kwa umri wako mzigo huu ni mkubwa na kwa umri wako vishawishi ni vingi vya marafiki, ndugu, jamaa na wengine, nafasi yako ile haina rafiki, haina ndugu, haina jamaa ni nafasi ya kulitumikia Taifa kwa hiyo nikutakie kila la kheri katika utumishi wako,” amesema Rais Samia.


