Na Winfrida Mtoi
Meneja Mkuu wa Simba SC, Dimitar Pantev, amethibitisha kuwa kipa Moussa Camara na Mohammed Bajaber wataikosa mechi dhidi ya Nsingizini Hotspurs kutokana na majeraha, huku akiwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuwa wamejipanga na wanajua wanachokwenda kufanya.
Kikosi cha Simba chenye wachezaji 22, kimeondoka leo kuelekea nchini Eswatini ambako kitaikabili Nsingizini Jumapili, Oktoba 19, 2025 katika mchezo wa raundi ya pili hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye dimba la Somhlolo.

Akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuondoka leo Oktoba 16, 2025 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam, Pantev amesema malengo yao ni kushinda mechi hiyo ya ugenini.
“Tunajua kwa nini tunakwenda huko, tunajua malengo yetu, matamanio yetu ni kushinda mechi hii. Morali ya timu ipo juu,” amesema.


