Na mwandishi wetu, Gazetini
BAADA ya kuing’oa Gaborone United ya Botswana, sasa Simba itaivaa Nsingizini Hotspurs ya Ligi Kuu ya Eswatini katika raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Nsingizini Hotspurs ilivuka hatua ya awali baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Simba Bhora inayoshiriki Ligi Kuu nchini Zimbabwe.
Katika mchezo wa kwanza, Nsingizi Hotspurs ikiwa nyumbani mjini Lilongwe, ilipata ushindi wa bao 1-0, kabla ya kufungwa kwa matokeo ya aina hiyo ilipokwenda ugenini.
Wekundu wa Msimbazi waliingia hatua ya pili kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Gaborone. Ilishinda bao 1-0 ikiwa ugenini, kabla ya sare ya bao 1-1 ilipowakaribisha Wabotswana hao jijini Dar es Salaam.
Mchezo wa kwanza kati yao na Nsingizini Hotspurs utachezwa kati ya Oktoba 17-26, mwaka huu, ambapo mshindi wa matokeo ya jumla atatinga hatua ya makundi.
Wapinzani hao wa Simba ni klabu yenye maskani yake mjini Nsingizini na ni klabu iliyoanzishwa mwaka 1984 lakini ilinyakua ubingwa wake wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita (2024–25).
Safari ya ubingwa ilihitimishwa na pointi zao 60 walizokusanya baada ya kushuka dimbani mara 26; walifunga mabao 44 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara 14 pekee.
Simba itakapokwenda ugenini itacheza na Nsingizini Hotspurs katika Uwanja unaomilikiwa na wenyeji wao hao wa Kumbukumbu ya Mfalme Sobhuza II unaopokea mashabiki 2,000.
Kwa sasa, timu hiyo inanolewa na aliyewahi kuwa kocha wa timu za vijana za Orlando Pirates, Mandla David Qhog, ambaye amechukua nafasi ya Simon Ngomane aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.
Katika kujiwinda na msimu huu wa Ligi ya Mabingwa, Nsingizini Hotspurs iliweka kambi nchini Afrika Kusini, ambapo ilicheza mechi kadhaa za ‘kutesti mitambo’, ikiwamo dhidi ya Mamelodi Sundowns.
Mikakati ya mabosi wa Nsingizini Hotspurs, akiwamo Mtendaji Mkuu, Banele Ngobe, imelenga kuiona timu hiyo ikitinga hatua ya makundi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Published:


