Na mwandishi wetu, Gazetini
MOJA ya vivutio vikubwa vya Uchaguzi Mkuu ujao wa Ivory Coast ni jina la mgombea wa urais, Simone Gbagbo, ambaye ni mke wa zamani wa aliyekuwa Rais wa Taifa hilo, Laurent.
Katika mazingira yasiyotarajiwa na wengi, bi. Simone atagombea nafasi hiyo ya juu zaidi akiwa na umri wa miaka 76.
Kwa ufupi, baada ya miaka mingi ya kusakamwa na wakati mwingine kulazimika kujificha ndani ili asikamatwe na vyombo vya dola, Simone atakabiliana na Rais Alassane Ouattara katika boksi la kura katika Uchaguzi wa mwezi ujao.
Simone anayefahamika kwa ujasiri wake, alikuwa kileleni mwa siasa za Ivory Coast wakati mumewe, Laurent, alipokuwa Rais wa nchi hiyo kuanzia mwaka 2000 hadi 2011.
Aidha, safari yake haikuanzia hapo. Msomi huyo wa Shahada ya Historia na Lugha alishirikiana na mumewe huyo kuupinga utawala wa dikteta Felix Houphouet-Boign katika miaka ya 1970.
Akisimulia katika moja ya mahojiano yake, Simone anasema: “Niliishia gerezani mara kadhaa, nilipigwa na wakati mwingine niliachwa wakidhani nimeshafariki.”
Mwaka 1982, wanandoa hao waliasisi Chama cha siasa cha FPI lakini miezi michache baadaye Laurent alikimbilia Ufaransa kutokana na kuandamwa na Serikali ya Houphouet-Boign.
Mwaka 1990, harakati zao zilifanikisha kuanguka kwa utawala wa miaka 33 wa Houphouet-Boigny. Ivory Coast ikafanya Uchaguzi wake wa kwanza tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ufaransa.
Laurent aliamua kugombea urais na bi. Simone akiwa mtu muhimu kwenye kampeni zake. Safari hii, walizidiwa kete na Houphouet-Boigny aliyeshinda kiti cha urais.
Mwaka 2000, Laurent alirejea kugombea tena kiti cha urais na kushinda. Ni baada ya jeshi kuwaondosha wagombea wote wa upinzani kwenye kinyang’anyiro.
Lakini, tofauti na alivyokuwa akipigania demokrasia, Laurent alibadilika na kuwa mtu tofauti baada ya kuingia madarakani.
Mkewe, Simone, alitajwa kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya jeshi, kiasi cha kulitumia katika kuwakaba koo wanasiasa wa upinzani na wakosoaji wengine.
Hali ya kisiasa ilikuwa mbaya zaidi baada ya Laurent kuhairisha mara sita Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kabla ya kukubali ufanyike mwaka 2010.
Hata aliposhindwa na Rais wa sasa, Alassane Ouattara, Laurent alikataa matokeo na kusababisha machafuko yaliyoua watu zaidi ya 3,000.
Wakati wote huo, Simone aliendelea kumkingia kifua mumewe, akidai kuwa anapaswa kubaki madarakani na si kumwachia Ouattara.
Wanajeshi waliokuwa wakimuunga mkono Ouattara wakishirikiana na Ufaransa walifanikiwa kuwatia nguvuni Simone na Laurent na huo ukawa mwisho wa vurugu zilizoitikisa Ivory Coast kwa miezi mitano mfululizo.
Kutokana na vurugu hizo, Simone alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani lakini Rais Ouattara alimtoa kwa nia ya kumaliza tofauti zao.
Kwa upande mwingine, Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) ilimfungulia mashitaka mwaka 2012 lakini nayo iliamua kuachana naye hapo baadaye.
Ni kama ilivyomfanyia Leurent. Baada ya kumshikilia kwa miaka saba nchini Uholanzi, iliamua kumuondoshea mashitaka hayo ya uhalifu wa kivita.
Aliporejea Ivory Coast, Laurent alimtwanga talaka Simone baada ya taarifa za kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwandishi wa habari, Nady Bamba.
Kuanzia hapo, Simone akawa na njia yake tofauti katika siasa, ikiwa ni pamoja na kuondoka katika Chama cha FPI na kuanzisha Movement of Capable Generations (MGC) anachokitumia sasa kusaka urais katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Published:


