THE HAGUE, Uholanzi
MAHAKAMA ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imehairisha usikilizaji wa mashitaka yanayomkabili Rais wa zamani wa Ufilipino, Rodrigo Duterte.
Kwa mujibu wa wanasheria wake, sababu ya kuhairishwa kwa kesi hiyo iliyopaswa kusikilizwa Septemba 23, mwaka huu, ni hali ya afya ya kiongozi huyo kuelezwa kutokuwa nzuri.
Duterte mwenye umri wa miaka 80, anashitakiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa oparesheni yake ya kudhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini humo, ikitajwa kuua maelfu ya raia.
Kile kilichoelezwa na wanasheria wake ni kwamba hali ya kiafya ya Duterte haimruhusu mwanasiasa huyo kusimama kizimbani wakati wa usikilizwaji wa mashitaka.
Historia inamtambua Duterte kuwa ni rais pekee wa zamani wa barani Asia kufunguliwa mashitaka na ICC.
Ikumbukwe, alikamatwa Machi, mwaka huu, mjini Manila, Ufilipino, na amekuwa chini ya ulinzi wa ICC nchini Uholanzi tangu kipindi hicho.
Wakati kesi yake iliposomwa kwa mara ya kwanza, ambapo alishiriki kupitia video, Duterte alionekana dhaifu na asiyemudu kuzungumza mara kwa mara.
Waendesha mashitaka wa ICC wanaamini kuwa operesheni yake ya kutokomeza dawa za kulevya ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 6,000 nchini Ufilipino.
Wakati huo huo, Rais wa sasa, Ferdinand Marcos, anakumbana na ukosolewaji mkubwa kwa madai ya kuhusika kwake katika kukamatwa kwa Duterte.
Published:


