9.2 C
New York

Xavi Simons; ‘Fundi’ wa La Masia aliyezikataa Chelsea, Man City

Published:

LONDON, England
WAMELAMBA dume! Kupitia usajili wa dirisha kubwa wa majira haya ya kiangazi barani Ulaya, Tottenham ilikamilisha dili la kumnasa kiungo wa kimataifa wa Uholanzi, Xavi Simons, kwa ada ya Pauni milioni 52.
Kinyume chake, hiyo haikuwa habari njema kwa matajiri wa klabu kubwa mbili za Ligi Kuu ya England (EPL), Chelsea na Manchester City, ambao walikuwa wakipigana vikumbo kuiwania huduma ya ‘fundi’ huyo.
Blues walikwama kumsajili baada ya kufika mezani na ofa ya Pauni milioni 47. Waliposhindwa kuelewana na Leipzig, ndipo walipomgeukia winga wa kimataifa wa Argentina kutoka Manchester United, Alejandro Gernacho.
Spurs, kwa upande wao, walihamishia nguvu zote kwa Simons baada ya kuwakosa Gibbs-White wa Nottingham Forest na Eberechi Eze aliyehamia Arsenal akitokea Crystal Palace.
Simons aliyetua Kaskazini mwa Jiji la London akitokea RB Leipzig ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), amesaini mkataba wa miaka mitano utakaombakiza klabuni hapo hadi mwaka 2030.
Aidha, mashabiki wa Leipzig wamebaki na kumbukumbu nzuri y mchango wake wa mabao 22 na ‘asisti’ 24 katika mechi 78 alizoshuka dimbani akiwa na jezi za timu yao.
Vilevile, Simons amezifumania nyavu mara tano katika michezo 28 akiwa na timu yake ya taifa ya Uholanzi tangu alipoanza kuitumikia wakati wa fainali zilizopita za Kombe la Dunia zilizofanyika kwa mara ya kwanza nchini Qatar.
Inafahamika kuwa uamuzi wa Leipzig kumuuza Simons ni katika kupunguza bajeti ya mishahara, ambapo staa huyo alikuwa akilipwa kitita cha Pauni milioni 9.5 kwa mwaka.
Maisha yalianzia La Masia
Safari ya maisha yake ya soka ilianzia katika kituo cha kuibua na kukuza vipaji vya soka cha La Masia kinachomilikiwa na klabu ya Barcelona.
Nyota huyo anayezungumza kwa ufasaha lugha za Kifaransa, Kiholanzi, Kihispania na Kiingereza, alijiunga na La Masia akiwa na umri wa miaka mitatu tu.
Akiwa bado hana jina kubwa, Simons aliutikisa ulimwengu wa kandanda baada ya kutajwa kuwa ndiye mchezaji bora zaidi duniani mwenye umri wa miaka 10.
Ndiyo, uwezo wake huo uliivutia kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike iliyompa dili la matangazo ya bidhaa zake akiwa na miaka 13.
Hata hivyo, alishindwa kujihakikishia namba katika kikosi cha kwanza cha timu ya wakubwa, hivyo akatimkia PSG akiwa na umri wa miaka 16.
Mambo hayakwenda vizuri jijini Paris, hivyo akapelekwa kwa mkopo PSV mwaka 2022 na huko ndiko alikoishawishi PSG kumrudisha mwaka 2019.
Hata hivyo, bado Simons hakuweza kupenya kikosi cha kwanza cha PSG, hivyo kutimkia kwa mkopo RB Leipzig ya Bundesliga, kabla ya klabu hiyo kumsajili moja kwa moja kwa Pauni milioni 43.
Anamkubali Neymar
Katika mahojiano yake mengi, Simons hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Neymar, akisema ndiye mchezaji aliyekuwa akimfutilia zaidi alipokuwa kinda wa La Masia, wakati huo Mbrazil huyo akiitumikia Barcelona.
Ikumbukwe, Simons aliposajiliwa na PSG mwaka 2029, alipata nafasi ya kutimiza ndoto yake ya kucheza na Neymar.
“Alinifahamu tangu nikiwa Barcelona na alikuwa kama baba yangu. Nitamshukuru mno kwa hilo. Nilikuwa na ndoto ya kucheza naye siku moja. Ni mtu muhimu sana kwangu,” alisema Simons.
Kwa upande mwingine, anasema alivutiwa pia na uchezaji wa Xavi Hernandez, Andres Iniesta na kiungo wa kimataifa wa Croatia, Luka Modric.
Apewa jezi ya heshima
Mkataba wake na Spurs una kipengele kinachoiruhusu klabu hiyo kumuongeza miaka miwili endapo itavutiwa na huduma ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 22.
Simons amekabidhiwa jezi namba 7 iliyokuwa inavaliwa na lejendari aliyeondoka klabuni hapo, Heung-Min Son, ambaye amejiunga na Los Angeles ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS).
“Kwa mwaka mmoja niliokuwa PSV, jezi namba 7 ilinipa mafanikio makubwa. Pia, ni jezi ninayovaa nikiwa na timu ya taifa. Ni chaguo sahihi. (Son) aliandika historia yake akiwa na jezi hii. Nadhani anastahili,” alisema Simons.
“Nimefurahi na nasubiri kwa hamu kuanza majukumu. Imekuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu. (Spurs) ni klabu kubwa na nilipokutana na kuzungumza na kocha, nikajua hapa ni sehemu sahihi kwangu.”
Faida tatu kwa Spurs
Kocha mpya wa Spurs, Thomas Frank, atanufaika na uwezo mkubwa wa Simons kucheza eneo la kiungo mshambuliaji (namba 10), hasa baada ya James Maddison na Dejan Kulusevski kupata majeraha ya goti.
Pia, katika mfumo wa 4-2-3-1, kocha Frank anaweza kumtumia Simons katika nafasi ya kiungo wa pembeni (winga) anayetokea upande wa kushoto mwa uwanja.
Akicheza maeneo hayo, Simons alikuwa na mchango mkubwa kwa Leipzig kwa misimu yote miwili aliyocheza klabuni hapo, akiwa na takwimu nzuri ya kutoa ‘asisti’ 18.
“Ni mchezaji mwenye kiu ya mafanikio. Ni mbunifu na ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga. Utulivu wake ndani ya boksi ni wa kiwango cha juu. Si mchezaji anayehitaji nafasi nyingi kufunga bao,” alisema kocha wake wa zamani katika klabu ya PSV, Fred Rutten.
Kama hiyo haitoshi, ni mchezaji mzuri pia katika majukumu ya ‘kukaba’. Kwa misimu miwili iliyopita, alikuwa ndiye mchezaji aliyepokonya mipira mara nyingi (51) kwenye eneo la ushambuliaji baada ya Florian Wirtz, Romano Schmid na Granit Xhaka.
Frank amezungumzia Simons akisema: “Nimefurahi kufanikisha usajili wake. Ni mchango mpya na muhimu kikosini. Ana umri mdogo lakini uzoefu wake ni mkubwa, amecheza mechi nyingi, tena kwa kiwango kikubwa.
“Xavi amethibitisha uwezo wake wa kufunga na kutoa asisti akiwa kwenye eneo la kiungo mshambuliaji na hata anapotokea pembeni. Pia, ni mzuri katika kuwaona wenzake na kuvuruga mabeki. Naamini atakuwa sehemu muhimu ya timu.”
Faida nyingine ya Simons ni kwamba si mchezaji mwenye rekodi ya majeraha ya mara kwa mara. Majeraha makubwa pekee ni yale ya kifundo cha mguu (enka) aliyopata katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool mwishoni mwa mwaka jana.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img