9.2 C
New York

Vigogo EPL ‘watatoboa’ msimu huu Ligi ya Mabingwa?

Published:

LONDON, Uingereza
KWA mara ya kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, timu sita za Ligi Kuu ya England (EPL) zitashiriki msimu huu wa michuano hiyo ya Shirikisho la Soka barani humo (UEFA).
Pia, ni kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2021-22, Ligi ya Mabingwa itazikosa timu kutoka Ligi Kuu ya Scotland baada ya Celtic na Rangers kushindwa kufuzu.
Droo ya mashindano hayo ilichezeshwa Agosti 28, mwaka huu, mjini Monaco, Ufaransa, ikiwa ni kwa msimu wa pili mfululizo kuchezwa kwa mfumo wa Ligi inayoshirikisha timu 36.
Mechi za mzunguko wa kwanza zitaanza kuchezwa Septemba 16, kabla ya mchezo wa fainali kupigwa Mei 30, mwakani.
Vigogo wa Ligue 1, PSG, watashiriki wakiwa ndiyo mabingwa watetezi wa taji walilobeba msimu uliopita kwa kuifunga Inter Milan mabao 5-0.
Arsenal
Msimu uliopita, Washika Bunduki walifika nusu fainali kwa mara ya kwanza tangu walipoigusa hatua hiyo miaka 16 iliyopita. Katika safari yao, waliitoa Real Madrid kwa kichapo cha jumla ya mabao 5-1.
Baada ya kumtegemea zaidi Mikel Merino msimu uliopita, Arsenal imeliongezea makali eneo la ushambuliaji kwa kuwasajili Victor Gyokeres, Eberechi Eze na Noni Madueke.
Chelsea
Blues, mabingwa wa Kombe la Dunia kwa ngazi ya Klabu na Conference League, wanarejea Ligi ya Mabingwa baada ya kuwa nje ya michuano hiyo kwa miaka miwili.
Hivyo, mabingwa hao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2021 wana rekodi ya kuwa timu pekee kubeba mataji yote manne ya UEFA.
Msimu huu, mashabiki wa Chelsea wana matumaini makubwa ya kufanya vizuri baada ya kocha Enzo Maresca kuimarisha kikosi kwa kuwanasa Joao Pedro, Liam Delap na Jamie Gittens.
Liverpool
Msimu huu, Liverpool watahitaji kupiga hatua zaidi. Ni baada ya wakali hao wa Anfield kuishia hatua ya 16 bora msimu uliopita, safari yao ikiishia mikononi mwa PSG.
Kama zilivyo timu zingine, Liverpool nayo ilikuwa ‘bize’ katika dirisha la usajili la majira haya ya kiangazi lililofungwa siku chache zilizopita.
Katika kuimarisha kikosi, kocha Arne Slot amewasajili Florian Wirtz, Jeremie Frimpong, Milos Kerkez, Hugo Ekitike, Giovanni Leoni na Alexander Isak.
Manchester City
Ukweli ulio wazi ni kwamba msimu uliopita ulikuwa mbaya kwa kocha raia wa Hispania, Pep Guardiola. Manchester City iliishia hatua ya 16 bora kwenye michuano hiyo.
Man City, mabingwa wa mashindano hayo mwaka 2023, watashiriki msimu huu wakiwa hawana huduma ya ‘fundi’ wao wa eneo la kiungo, Kevin de Bruyne.
Hata hivyo, Guardiola ameingia sokoni na kuwasajili Rayan Cherki, Rayan Ait-Nouri na Tijjani Reijnders, akiamini wataiwezesha Man City kuwa na kiwango bora msimu huu wa Ligi ya Mabingwa.
Newcastle United
Matajiri wapya wa EPL. Vijana hao wa kocha Eddie Howe walirejea Ligi ya Mabingwa msimu wa 2023-24 baada ya kuwa nje ya michuano hiyo kwa miaka 20.
Newcastle ilifanya vizuri katika mechi zake za hatua ya makundi, ikiwamo kupata ushindi mnono wa mabao 4-1 walipokutana na wakali wa Ligue 1, PSG.
Je, watakuwa kwenye kiwango bora cha ushindani hata baada ya kuwapoteza Hugo Ekitike, Joao Pedro na Isak?
Tottenham
Spurs watashiriki Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2024-25. Timu hiyo ya Kaskazini mwa London ilimaliza msimu uliopita ikiwa na taji la Ligi ya Europa.
Chini ya kocha mpya aliyetokea Brentford, Thomas Frank, ilipoteza taji la kwanza msimu huu, ilipofungwa kwa penalti na PSG katika mchezo wa Super Cup.
Frank ameimarisha kikosi chake kwa kuwasajili nyota watatu wa viwango vikubwa. Wachezaji hao ni Joao Palhinha, Mohammed Kudus na Xavi Simons aliyekuwa tishio Bundesliga akiwa na RB Leipzig msimu uliopita.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img