9.8 C
New York

Jeshi Mali na jaribio la kupindua Serikali

Published:

BAMAKO, Mali

HALI ya taharuki imeibuka nchini Mali baada ya wanajeshi takarbani 50 kushikiliwa kwa madai ya kusuka mpango wa kuipindua Serikali inayoliongoza Taifa hilo la Afrika-Magharibi. Wanajeshi hao, wakiwamo wawili wa ngazi za juu, wamekamatwa kwa madai ya kutaka kumng’oa madarakani kiongozi wa kijeshi, Luteni Kanali Assimi Goita.

Miongoni mwa waliokamatwa ni aliyewahi kuwa kiongozi wa jeshi mjini Mopti, Abass Dembele, ambaye alikamatwa akiwa nyumbani kwake. Mwingine ni mwanamama mwenye nafasi ya juu jeshini, Jenerali Nema Sagar. Miongoni mwa maofisa wanawake wachache wa jeshi waliopigana vita mwaka 2013.

Tangu mwaka 2012, jeshi la Mali limekuwa kwenye mapigano na makundi ya waasi Kaskazini mwa nchi hiyo. Miongoni mwa makundi hayo ni Jama’at Nasr al-Islam wal-Muslimin (JNIM). Kwa mujibu wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch, vita hiyo imesababisha vifo zaidi ya 1,000, huku watu 350,000 wakilazimika kuyakimbia makazi yao.

Miji mingi ya Kaskazini inashikiliwa na waasi, ambapo wamekuwa wakizuia upatikanaji wa huduma muhimu kwa wananchi. Wakati anaingia madarakani mwaka 2021, kiongozi wa kijeshi, Goita, aliahidi kurejesha hali ya usalama nchini humo. Licha ya jitihada zake za kushirikiana na Ufaransa iliyopeleka maelfu ya wanajeshi nchini Mali, bado hajaonekana kufaulu.

Hata hivyo, utawala wa kijeshi wa Goita umekuwa ukikosolewa vikali, hasa baada ya kupitisha sheria inayomruhusu kiongozi huyo kubaki madarakani kwa muda atakaotaka, tena bila kuhitaji Uchaguzi Mkuu. Amepuuzia ahadi yake ya mwaka jana, kwamba jeshi lingewapa wananchi haki ya kuchagua viongozi.

Mbaya zaidi, Serikali ya kijeshi imefuta vyama vya siasa, pia ikipiga marufuku mikutano ya kisiasa.
Hivi karibuni, Waziri Mkuu wa zamani wa Taifa hilo, Moussa Mara, alikamatwa na kufunguliwa mashitaka ya kuipuuza Serikali, hatua iliyokuja baada ya ziara yake ya kuwatembelea wafungwa gerezani.

Pia, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Choguel Maiga, ambaye amekuwa akiikosoa Serikali ya Goita, anakabiliwa na mashitaka ya rushwa na uchunguzi unaendelea. Wakati Serikali ikiendelea ‘kuwashughulikia’ wakosoaji, bado suala la usalama wa raia limeonekana kuwa changamoto iliyokosa ufumbuzi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img