1.7 C
New York

Visual| Mapambano ya VVU Tanzania na mchango wa PEPFAR

Published:

Na Mwandishi Wetu, Gazetini

Ikiwa ni zaidi ya miaka 40 sasa tangu kuwapo kwa janga la Virusi Vya UKIMWI, Serikali ya Tanzania imesema kuwa imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 58 kutoka 130,000 mwaka 2003 hadi 54,000 mwaka 2021 kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR).

Hayo yamebainishwa Februari 2, 2023 na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 20 ya mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yaliyowezeshwa na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) iliyofanyika katika Hoteli ya Serena Dar es Salaam.

Amesema kuwa kupitia mfuko huo ambao umeleta mabadiliko makubwa katika katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi umesaidia kupunguza vifo kwa asilimia 76 kutoka 120,000 mwaka 2003 hadi 29,000 mwaka 2021.

Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuunga mkono mpango huo katika kujenga miundombinu ya afya, kutoa mafunzo, kutoa vifaa vya uchunguzi na vifaa vya kinga binafsi, na kuanzisha mifumo ya kufuatilia maambukizi.

“Serikali ya Tanzania inafahamu kwamba, Serikali ya Marekani ni mshirika mkubwa katika kukabiliana na Virusi vya Ukimwi nchini Tanzania, ikiwa imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.6 kwa ajili ya kukabiliana na janga hiyo,” amesema Majaliwa.

Kadhalika, Majaliwa amesema kuwa PEPFAR kwa sasa unasaidia zaidi ya watu milioni 1.5 wanaoishi na VVU (WAVIU) kwenye matibabu kupitia mpango wa kuokoa maisha wa ARVs ambapo kabla ya kuanzishwa kwake WAVIU wasiozidi 1,000 ndio walikuwa kwenye Tiba ya Kupambana na Virusi vya Ukimwi.

Amesema kuwa Serikali ya Tanzania inajivunia kushirikiana na Serikali ya Marekani kupitia PEPFAR kufikia malengo ya 95/95/95 ifikapo mwaka 2025.

“Hivi sasa kupitia mpango wa PEPFAR tunatekeleza tafiti ya athari za VVU Tanzania kwa mwaka 2022-2023 ambao unakusudiwa kutoa taarifa muhimu katika kuandaa mikakati ya kuzuia maambukizi mapya na kuhakikisha watu wanajua hali zao za VVU,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Naye, Mkurugenzi Mkazi wa PEPFAR Tanzania, Jessica Greene amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana bado kuna kazi kubwa ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma unaongezwa kwa wasichana, wanawake vijana, watoto na makundi ya jamii yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa VVU.

Tangu kuanzishwa kwa PEPFAR mwaka 2003, chini ya utawala wa Rais George W. Bush, Serikali ya Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 100 katika kupambana na VVU/UKIMWI duniani kote, ikijumuisha takriban Dola za Kimarekani bilioni saba zilizotolewa Tanzania.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img