1.4 C
New York

Makala: Wazazi, wadau wataka fursa nyingine waliokatizwa masomo kwa mimba

Published:

CHANGAMOTO za maisha ikiwamo ukosefu wa mahitaji muhimu kwa wasichana walioko shule ni moja ya vichochezi vinavyosababisha wengi kuishia kupata ujauzito hali inayokosesha fursa ya kuendelea na masomo.

Hali hiyo imefanya ndoto za baadhi ya wasichana ngazi ya elimu msingi na sekondari kuishia njiani kwani hujikuta wakifukuzwa shule kutokana na kupata mimba.

Ingawa katika miaka ya hivi karibuni mwamko wa kuwalinda na kuwasaidia wasichana dhidiya vichochezi vya mimba za utotoni umekuwa mkubwa, bado hali siyo ya kufurahisha sana, kwani kuna kundi kubwa linalokatisha masomo kutokana na mimba.

Takwimu za msingi zinzotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) BEST zilizotolewa mwaka 2019, kuna ongezeko la asilimia 57 la wanafunzi wa seekondari walioacha shule kwa kupata ujazito mwaka 2019 hadi kufikia  wasichana 5,398 kutoka wasichana 3,439 mwaka 2015.

Aidha, kwa mujibu wa takwimu hizo, hali ilikuwa ni mbaya zaidi kwa kidato cha pili na cha tatu.

Wanafunzi walioacha shule kwa kupata ujauzito wakiwa kidato cha pili mwaka 2019 walikuwa 1,536 wakifuatiwa na kidato cha tatu ambao walikuwa 1,527.

Pia katika kidato cha nne wanafunzi 1,331 waliacha masomo kwa ujauzito huku kwa kidato cha kwanza ikiwa ni 880.

Kwa upande wa kidato cha tano kulikuwa na wanafunzi 81 huku cha sita wakiwa ni 43.

Tafasri yake ni kwamba wasichana wengi wanashindwa kuvuka kidato cha pili na cha tatu kutokana na ujauzito.

Kulingana na ripoti hiyo, ujauzito kwa wasichana  ilikuwa ni sababu ya pili iliyochochea wanafunzi kukatisha masomo kwa asilimia 5.5 ikitanguliwa na ile ya utoro ambayo ilikuwa asiliami 91.6.

Aidha, mkoa wa Morogoro kwa mwaka 2019 wanafunzi walioacha shule kwa ujauzito walikuwa 389 ukiwa ni miongoni mwa mikoa yenye takwimu za juu zaidi.

Mwajuma Iddi (17) halisi, ni miongoni mwa wasichana wa Kitanzania aliyekumbana na kadhia hiyo ya kukatisha masomo yake kwa sababu ya ujauzito.

Mwajuma ambaye anaishi na bibi na babu yake wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, anasema bahati mbaya hiyo ilimkuta akiwa kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari ya Mazinyungu mwaka 2018.

Anaeleza kuwa, alipokutana na mwanaume ambaye alimlaghai na kumpachika ujauzito ambao ulipeperusha kabisa ndoto yake ya kuwa mwanasheria.

Mwajuma ambaye ni mtoto wa kwanza kati ya watano wa mama yake, anasema kwa sasa anaishi na babu yake lakini maisa siyo rahisi kama alivyokuwa akifikiria mwanzo.

Machungu na majuto anayopitia ni kutelekezwa na  mwanaume aliyempa ujauzito,kwani baada ya mkasa huo muhusika wa mimba hiyo alitoweka kabisa mjini Kilosa.

“Mwanangu huyu ambaye ana miaka 2 na miezi 3 namlea mwenyewe kwani baba yake alikimbia kusiko julikana. Niliambiwa tu hayupo tena hapa Kilosa, hivyo nabaki tu kusema kwamba ningejua.

“Nakumbuka Septemba mwaka jana mwanangu alilazwa hospitali akaandikiwa sindano 10 na kila sindano Sh 2,500, sikuwa na fedha niliwaza sana nikasema kama nisingefanya ule upuuzi leo nisingekuwa hapa, hivyo sitaki kabisa mwanangu apitie haya niliyoyapitia,” anasema Mwajuma.

Mwajuma anasema, iwapo atapata fursa nyingine ya elimu ataitumia kikamilifu kwani pamoja na kwamba ana furaha ya kuwa na mtoto, lakini haoni dira ya maisha yake.

“Ikitokea nimepata fursa nyingine ya elimu kwa kweli nipo tayari kusoma kwani pamoja na kumfurahia mwanangu lakini nikiangalia masisha haya tunayoishi na babu na bibi nakosa kabisa furaha,” anasema Mwajuma.

Babu yake wajuma, anayefahamika kama Mzee Kassim Issa Yusufu, anasema anatamani kuona mjukuu wake akirudi shule na kupata ujuzi wowote kwani maisha ni magumu.

“Majukumu ni mazito sana ndiyo maana kila siku naomba dua itokee fursa aende akapate ujuzi wowote iwe charahani au ujuzi wowote kwani hapa ananipa matatizo tu,” anasema Mzee Yusufu.

Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi BEST kwa mwaka 2019 pekee wilaya hiyo ya Kilosa ilikuwa na jumla ya wasichana 94 waliokatisha masomo kutokana na mimba, ikishika nafasi ya tatu kwenye zile zilizokuwa na takwimu za juu kwa wasichana kupata ujauzito wakiwa shule. Wilaya hiyo ilitanguliwa na wilaya za Geita(105) na Dodoma DC(96).

Mei 11, mwaka huu, Selikali kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, akiwa katika shule ya Sekondari ya Kibasila jijini Dar es Salaam alisema serikali imekuja na utaratibu maalumu wa kusaidia wanafunzi wanaopata ujauzito wakiwa shuleni.

Kwa mujibu wa Prof. Ndalichako mfumo huo wa elimu mbadala unafadhiliwa na serikali ya Uingereza.

“Tumeweka utaratibu kwa watoto ambao wanapata ujauzito kuendelea na masomo yao kupitia njia ya elimu mbadala.

“Katika mfumo huo itategemea mwanafunzi ameacha shule akiwa kiwango gani, lakini kama ameacha kwa mfano akiwa kidato cha kwanza anaweza akasoma kupitia mfumo wa elimu mbadala na akifanya mtihani wake wa kidato cha pili akafaulu basi kidato cha tatu ataendelea katika mfumo wa kawaida (rasmi).

“Vilevile kwa kidato cha tatu akifanya mtihani wa kidato cha nne katika mfumo usio rasmi na akafaulu basi atapangiwa shule yoyote kwenye utaratibu rasmi.

“Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kuwa tunasimamia elimu kwa watoto wa kike na kuondoa vikwazo ambavyo vinasababisha watoto wa kike wasifanye vizuri katika masomo yao sambamba na kuboresha elimu kwa ujumla ili watoto wa kike na wakiume wapate elimu iliyobora,” alisema Prof. Ndalichako.

Wadau wataka mpango uharakishwe

Aidha, katika kutoliakkazo hilo, wadau wa Haki za Watoto nchini wameiomba serikali kupitia wizara ya elimu kuhuisha mchakato wa kuwarejesha shuleni wasichana wanaopata ujauzito.

Akizungumza Juni 16, mwaka huu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika wakati mashirika 13 yanayotetea  haki za watoto yalipofanya maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, amesema Mashirika hayo yametoa mapendekezo sita kwa serikali ikiwemo suala la mtoto wa kike kurejea shule baada ya kujifungua.

“Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika sisi taasisi zinazotetea haki za watoto na wasichana tunasema katika masuala yanayohusu makundi haya ni vema serikali kuangalia nini matakwa ya kundi hili na kuwafanya kuwa sehemu ya kutatua changamoto hizo.

“Wasichana wamekuwa wakifukuzwa shule kwa sababu ya kupata ujauzito kwa kufuata taratibu ambazo hazina nguvu ya sheria, bali kupitia taratibu zilizozoeleka.

“Pamoja na serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya elimu kuzuia mimba za utotoni bado mtoto wa kike anakosa huduma saidizi pale anapopewa ujauzito na kuondolewa katika mfumo rasmi wa elimu.

“Licha ya hivi karibuni kuwapo kwa jitihada za serikali kutoa fursa kwa mabinti kuendelea na masomo kupitia mifumo mbadala kama MEMKWA bado mifumo hii haijengi usawa kwa kumlazimisha msichana kutumia mifumo mbadala, tofauti na inavyofanywa Zanzibar,” aanasema Rebecca.

Anaongeza kuwa, wao kama wadau wataendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ili kuwa na jamii na taifa imara lenye kujali haki na ustawi wa watoto, hasa wa kike.

Wazazi

Wazo la serikali pia linaungwa mkono na Mzee Zonobi Mwanambula ambaye ni Mwenyekiti wa kitongoji cha Behewa, Kata ya Kasiki.

Anasema mpango wa serikali kuwapa nafasi ya pili wasichana kurejea shule utaleta manufaa chanya kwa jamii kwani itatengeneza fursa nyingine kwa mabinti hao.

“Iwapo serikali itakuja na mpango huu ni bayana kwamba utakuwa ni msaada mkubwa kwa mabinti zetu kwani siyo wote wanaopata ujauzito inakuwa ni kwa kutaka. Wengine wanabakwa na mambo mengine kama hayo, hivyo ni wazo zuri kwa serikali,” anasema Mwanambula.

Mwajuma Kassim (65) mkazi wa Dumila mkoani Morogoro ni miongoni mwa wazazi wanaounga mkono hoja ya mabinti kupatiwa fursa nyingine ya kupata elimu nchini.

“Kwa kweli serikali itilie mkazo hili la elimu kwani wasichana wanaopata ujazito ni wengi sana hivyo ukisema hawa wote wabaki tu mtaani haitakuwa na afya kwa taifa,” anasema Mwajuma.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img