Na mwandishi wetu, Gazetini
SIKU chache zilizopita, maofisa waandamizi wa jeshi nchini Guinea-Bissau walitangaza kuipindua Serikali ya Rais Umaro Sissoco Embalo. Ni hatua iliyofuatiwa na kitendo cha Jenerali wa jeshi kuapishwa na kuanza majukumu ya urais.
Uamuzi wa jeshi kuchukua nchi ulitokana na sarakasi nyingi za Uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, ikiwamo baadhi ya wagombea wa upinzani kupigwa ‘stop’ kuwania nafasi ya kwenda Ikulu.
Kabla ya jeshi kutangaza kuingia Ikulu, Embolo alikuwa akiwania muhula wake wa pili tangu alipoingia madarakani mwaka 2019.
Kwa upande mwingine, matukio ya jeshi kupindua serikali si mapya katika historia ya siasa za Guinea-Bissau. Makala haya yanachambua zaidi.
Akiwa Waziri Mkuu, Joao Bernardo Vieira alishirikiana na baadhi ya vigogo wa jeshi na kufanikiwa kumpindua Rais Luis Cabral mwaka 1980.
Miaka mitano baadaye, baadhi ya maofisa waandamizi wa jeshi walikamatwa wakishutumiwa kusuka mpango wa kumpindua Vieira. Sita kati yao walinyongwa na wengine walifariki wakiwa mahabusu.
Juni, 1998, lilifanyika jaribio jingine la kumpindua Vieira, ambalo lilishindikana lakini lilisababisha machafuko makubwa nchini humo.
Hatimaye Vieira aliondoshwa kwa mapinduzi ya kijeshi ya Mei, 1999. Aliyeongoza mapinduzi hayo ni Jenerali Ansumane Mane.
Mapinduzi mengine ni yale ya Septemba, 2003, ambayo yalimuondoa Rais aliyechaguliwa kwa kura za wananchi, Kumba Yala.
Itakumbukwa kuwa Yala aliingia madarakani akiwa chaguo la wananchi baada ya marais wawili wa mpito tangu Vieira alipopinduliwa.
Lakini, Yala hakuwa na mahusiano mazuri na Jenerali Mane. Vikaibuka vita vilivyosababisha kifo cha Jenerali huyo.
Aidha, Yala naye alipinduliwa mwaka 2004, mapinduzi yaliyoongozwa na Jenerali Verissimo Correia Seabra, ambaye hata hivyo aliuawa miezi michache baadaye.
Henrique Rosa aliingia Ikulu akiwa Rais wa mpito hadi mwaka 2005, ambapo Vieira alirudi madarakani kupitia Uchaguzi Mkuu.
Miaka minne baadaye, Vieira aliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi waliotajwa kuwa watiifu kwa Jenerali Batista Tagme Na Waie.
Siku moja kabla ya Vieira kupigwa risasi, Jenerali Na Waie aliuawa kwa bomu, hivyo Raimundo Pereira akaingia madarakani kuwa rais wa mpito wa Guinea-Bissau.
Pereira aliondoka madarakani na kumpisha Malam Bacai Sanha aliyechaguliwa kwa kura za wananchi katika Uchaguzi Mkuu. Alifariki kwa ugonjwa akiwa madarakani, hivyo jeshi kurudi madarakani Aprili, 2012.
Mwaka 2022, akiwa ameingia madarakani mwaka 2019, Rais Umaro Sissoco Embalo alinusurika kupinduliwa baada ya wanajeshi wenye silaha kuvamia makazi yake.
Mwishoni mwa mwaka 2023, Embalo alivunja Bunge kwa madai kuwa zilikuwepo njama za kuipindua Serikali yake. Alidai amenusurika katika majaribio matatu.
Oktoba, mwaka huu, jeshi lilitangaza kuwashikilia maofisa wake kadhaa kwa madai ya kupanga jaribio la kuipindua Serikali. Novemba 26, ikatimia baada ya jeshi kutangaza kuingia Ikulu na kumuweka kando Embalo.
Published:


