7.8 C
New York

Kilichomponza Waziri Mkuu aliyehukumiwa kifo

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
WAZIRI Mkuu wa zamani wa Bangladesh, Sheikh Hasina, amehukumiwa kifo baada ya kukutwa na hatia katika mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu wakati wa maandamano yaliyomng’oa madarakani mwaka jana.
Hukumu hiyo ilisomwa Jumatatu ya wiki hii na Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya Bangladesh ikimtaja mwanasiasa huyo kuhusika katika mauaji ya maelfu ya waandamanaji.
Kwa upande mwingine, pia Mahakama hiyo imemuhukumu kifo Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Hasina, Asaduzzaman Khan, wakati aliyekuwa Mkuu wa Polisi atatumikia kifungo cha miaka mitano gerezani.
Serikali ya mpito inaongozwa na Muhammad Yunus, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi na mshindi wa tuzo ya Nobel, huku Uchaguzi Mkuu ukitarajiwa kufanyika Februari, mwakani.
Maandamano yaliyomng’oa madarakani
Kwa mujibu wa kile kilichoelezwa mahakamani, akiwa Waziri Mkuu, aliamrisha vyombo vya Dola kutekeleza mauaji wakati wa maandamano hayo yaliyoongozwa na wanafunzi.
Inaelezwa kuwa vyombo vya dola vilitumia risasi za moto, ndege zisizo na rubani na hata helikopta kuwashambulia waandamaji. Pia, baadhi yao walikamatwa na kunyongwa.
Katika maandano hayo, watu zaidi ya 1,400 waliopoteza maisha na wengine 25,000 kujeruhiwa, kwa mujibu wa ripoti ya Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR).
Apinga hukumu akiwa mafichoni
Hata hivyo, Hasina ambaye alikuwa madarakani tangu mwaka 2019, hakuwepo mahakamani wakati hukumu ya kifo ikisomwa. Amekuwa akiishi uhamishoni nchini India tangu Serikali yake ilipotolewa madarakani.
Akitumia mitandao ya kijamii, Hasina amekosoa humu hiyo alisema: “Nakanusha madai yote ya ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi yangu. Najivunia historia nzuri ya Serikali yangu katika kulinda haki za binadamu na maendeleo.
Kwa sasa, Serikali ya mpito ya Bangladeshi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, imetuma maombi rasmi kwa India, ikitaka Hasina kurejeshwa nyumbani ili kutumikia hukumu yake ya kifo.
“Ni jukumu la India kutekeleza sharti hili la mkataba (wa kumkabidhi Hasina) uliopo kati ya mataifa haya mawili,” ilieleza ripoti ya Wizara, ingawa India haijatoa msimamo wake.
Sheria ziko wazi, kwamba Hasina, licha ya kukana mashitaka, hawezi kukata rufaa hadi pale atakapojisalimisha au kukamatwa ndani ya siku 30 baada ya hukumu kusomwa.
Kuelekea Uchaguzi Mkuu
Wakati huo huo, baadhi ya wachambuzi wanadhani huenda Uchaguzi Mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Februari, mwakani, ukagubikwa na vurugu. Kwanini?
Chama cha Awami League, ambacho ndicho anachotokea Hasina, kimefungiwa kushiriki masuala ya siasa, hatua ambayo imeibua hasira kwa wanachama wake.
Mtoto wake wa kiume, Sajeeb Wazed, ambaye anaishi Marekani, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa wafuasi wa Chama hicho watafanya kila linalowezekana kuzuia Uchaguzi endapo hakitaruhusiwa kushiriki.
“Hatutaruhusu Uchaguzi bila Awami League kushiriki. Maandamano yetu yataendelea kuimarika, tutafanya chochote kinachowezekana. Kama jumuhiya za kimataifa zitakaa kimya, basi zitatokea vurugu kabla ya Uchaguzi,” amesema.
Historia fupi
Hasina ni mtoto wa kwanza wa kike wa muasisi wa Taifa la Bangladesh, Sheikh Mujibur Rahman. Hasina na dada yake walikimbia nchini humo baada ya baba, mama na kaka zake watatu kuuawa na wanajeshi waliopindua Serikali mwaka 1975.
Hasina alirejea Bangladesh mwaka 1981 na kuwa kiongozi wa Chama cha siasa cha baba yake, Awami League. Baada ya miaka mitano ya kuwa upinzani, Chama hicho kilishinda Uchaguzi wa mwaka 1996 na Hasina akawa Waziri Mkuu.
Alirejea madarakani mwaka 2009, hadi pale wanafunzi waliochoshwa na hali ngumu ya maisha walipoingia barabarani na kumng’oa madarakani mwaka jana.
Katika utawala wake, jumuhiya za kimataifa zilikosoa zaidi uminywaji wa demokrasia, wakionya kuwa Hasina hakutaka upinzani, na badala yake akitamani kuona Bangladesh ikiwa na chama kimoja, Awami League.
Utawala wake ulisifika kwa kuwandamiza wanasiasa wa upinzani, kuminya uhuru wa vyombo vya habari, ambapo waandishi walikamatwa na kufunguliwa mashitaka, pia kashfa za rushwa zikitawala katika taasisi za Serikali.
Leo hii, si tu Hasina, bali sehemu kubwa ya ndugu na viongozi wenzake wa Serikali, akiwamo Khan, wanaishi nje ya nchi wakikimbia mashitaka na hasira za wananchi.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img