25.9 C
New York

Historia ya Afrika na tuzo ya Amani ya Nobel

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
TANGU kuanzishwa kwake mwaka 1901, Tuzo ya Amani ya Nobel imekuwa ikiheshimiwa duniani kote, ikitambua jitihada za watu au taasisi katika kupigania amani, usawa au haki za binadamu.
Kwa mwaka huu, mwanasiasa wa Venezuela, Maria Corina Machado, ndiye aliyechukua tuzo hiyo kwa juhudi zake za kupambania demokrasia nchini humo.
Hata hivyo, Afrika nayo haiko nyuma. Kwa nyakati tofauti, Bara hilo limetoa washindi wa tuzo hiyo ya Amani ya Nobel, ikianzia mwaka 1960 alipoichukua Albert Luthuli.
Luthuli alitangazwa kuwa mshindi wa tuzo hiyo kutokana na harakati zake za kupinga vitendo vya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini.
Anwar Sadat wa Misri naye aliingia kwenye historia baada ya kupewa tuzo hiyo mwaka 1978, akiheshimishwa kwa jitihada zake za kufanikisha mkataba wa amani kati yao na Israel.
Baada ya Sadat, Afrika Kusini iliwashuhudia Desmond Tutu (1984), Nelson Mandela na F.W. de Klerk (1993) nao wakishinda tuzo hiyo.
Mwaka 2001, tuzo ilielekea Ghana kwa Kofi Annan, akitunukiwa kwa kazi nzuri ya kuhamasisha amani duniani akiwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).
Afrika Mashariki iliandika historia ya kuwa sehemu ya tuzo hizo baada ya mwanaharakati wa Kenya, Wangari Maathai, kuitwaa mwaka 2004.
Mwaka 2011, Ellen Johnson Sirleaf na Leymah Gbowee, walitangazwa kuwa washindi wa pamoja kwa mchango wao wa kuhamasisha wanawake kushiriki katika kulinda amani nchini Liberia.
Kwa miaka ya hivi karibuni, 2018 na 2019, Afrika imewashuhudia Denis Mukwege kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed Ali, nao wakipewa tuzo hiyo.

Related articles

Recent articles