12.5 C
New York

Nauza kura yangu, nani atafika bei Oktoba 29?

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
KAMPENI zimeshika kasi. Ni siku chache tu zimebaki kuelekea Oktoba 29, siku ambayo Watanzania watatumia haki yao ya Kikatiba kupiga kura na kuchagua rais, wabunge na madiwani.
Ni wakati huu wa kampeni, tumeshuhudia vyama vya siasa vikipishana mikoani kuwanadi wagombea wake wa nafasi hizo. Kwa ufupi, mikutano ya kampeni na ahadi za wagombea vimefunika na kuiweka kando mijadala yote ya siasa hapa nchini.
Binafsi, niweke wazi, kwamba nitaiuza kura yangu, tena kwa ‘gharama’ kubwa. Mgombea atakayefika bei ndiye nitakayempa kura yangu. Kinyume cha hapo, nitampa mpinzani wake atakayekuwa tayari kufikia gharama za kura yangu.
Ndiyo, kwa kipindi kama hiki, kila mgombea anaihitaji kura yangu. Kwanini niitoe bure, kana kwamba sijui umuhimu wake? Nitaiuza, tena kwa bei nitakayo.
Siyo dhambi. Kama unaelewa umuhimu wa kura yako, kama nilivyo mimi, huwezi kuigawa bure. Huwezi kupoteza muda wako kumpa kura mgombea ambaye hafiki bei ya kura yako. Iko hivyo.
Sasa jiulize; zikiwa zimebaki siku chache tu kulielekea boksi la kura, unaijua gharama halisi ya kura yako ili usiigawe bure kama wengine?
Nikwambie tu; kama huijui gharama ya kura yako utashindwa kupanga bei uitakayo mbele ya mgombea yeyote atakayekufuata, awe wa nafasi ya urais, ubunge au udiwani.
Matokeo yake, hutonufaika kwa kuiza kura yako kipindi hiki cha Uchaguzi na badala yake wagombea watakutumia kama daraja la kuwapeleka madarakani. Je, ni ipi gharama halisi ya kura yako?
Gharama halisi ya kura yako ni namna ulivyotumia kipindi cha kampeni kusikiliza, kuelewa na kupima sera za wagombea mbalimbali, bila kujali itikadi ya chama cha siasa.
Ukiweka kando mapenzi ya chama au mwanasiasa fulani, ni sera zipi zilizokuvutia ukiamini zinatekelezeka na zina tija katika ustawi wa jamii inayokuzunguka.
Kimsingi, mwananchi wa aina hii ndiye bei halisi ya kura. Ndiye anayeiuza kura yake. Ikimaanisha, kura yake italeta tija kwa kuchagua kiongozi atakachagiza mabadiliko katika jamii yake.
Kinyume chake, mwananchi ambaye hakusikiliza, hakuelewa na wala hakupima sera za wagombea, kura yake haina gharama. Ataishia kuigawa bure kwa msukumo wa mapenzi aliyonayo kwa chama au mwanasiasa fulani.
Je, utaiuza kura yako au unakwenda kuigawa bure? Je, uamuzi wako wa kukichagua chama au kumpigia kura mgombea fulani utatokana na kusikiliza, kuelewa na kupima sera zake, au ni mapenzi binafsi uliyonayo kwake?
Oktoba 29, twendeni tukauze kura zetu na si kuzigawa bure kama ‘mazuzu’. Mungu ibariki na ilinde Tanzania yetu!

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img