LONDON, Uingereza
MAPENZI yake yasiyo na mfano kwa Manchester United yalianza baada ya klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.
Ni kutokana na mapenzi tu, Marin Zdravkov Lavidzhov ambaye ni fundi ujenzi nchini Bulgaria, alifuata sheria zote za kubadili jina na kujiita ‘Manchester United’.
Hakuishia hapo. Lavidzhov alikuwa na paka wake. Naye aliamua kumpachika jina la David Beckham, ambaye wakati huo alikuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha Manchester United.
Kama hiyo haitoshi kuonesha mapenzi yake kwa Manchester United, Lavidzhov hakuona shida kujichora ‘tattoo’ ya nembo ya klabu hiyo katika paji la uso, ambayo alikuwa nayo hadi alipofariki hivi karibuni akiwa na umri wa miaka 62.
Nyumbani kwake huko Bulgaria ni kivutio cha mashabiki wa soka kwa namna kulivyopambwa na jezi, mabango na picha za Manchester United, zikiwamo za wachezaji aliowapenda. Miongoni mwao ni Dimitar Berbatov, ambaye pia ni raia wa Bulgaria.
Baada ya taarifa za kifo chake, klabu ya Manchester United kupitia kwa Msemaji wake, ilituma ujumbe unaosomeka: “Tunasikitika kusikia habari hii na tunatuma salamu zetu za rambirambi kwa familia na marafiki zake.”
Lavidzhov alipata wazo la kujiita Manchester United mwaka 1999 baada ya klabu hiyo kuifunga Bayern Munich mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa.
Hata hivyo, haikuwa rahisi. Mchakato wa kisheria ulichukua muda mrefu, kabla ya kufanikiwa mwaka 2014 na kuanza kujiita kwa jina hilo.
Kwake yalikuwa ni mafanikio makubwa, kiasi cha kujipongeza kwa kujichora tattoo ya nembo ya Manchester United katika paji la uso.
Kutokana na upekee wa mapenzi yake kwa Manchester United, Gazeti la Sun lilimwezesha kutembelea Uwanja wa Old Trafford mwaka 2014. Ni umbali wa maili 4,000 kutoka nchini kwake, Bulgaria.
Ukiachana na hiyo, pia Lavidzhov alipewa tiketi ya bure ya kwenda kuitazama Manchester United ikiwa ugenini katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Sunderland.
Tukio la kusisimua zaidi na kusababisha amwage machozi, ni pale Lavidzhov aliporuhusiwa kuingia kwenye chumba cha kubadilishia.
“Nitaikumbuka siku hii milele na nitawasimulia familia na marafiki zangu katika siku zote za maisha yangu,” alisema baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Msimu huo, Manchester United ilimaliza mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ikiwa nafasi ya pili, nyuma ya majirani zao, Manchester City, waliotwaa ubingwa.
Published:


