22 C
New York

Huyu ndiye kocha mpya Yanga

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini
YANGA wamemtambulisha kocha mpya, Patrick Mabedi, ambaye amejiunga na benchi la ufundi kufanya kazi chini ya Romain Folz. Ifahamike kuwa Yanga inakuwa klabu yake ya tano akihudumu katika nafasi ya msaidizi wa kocha mkuu.
Kabla ya kujiunga na Wanajangwani, beki huyo wa zamani aliwahi kuwa kocha msaidizi katika klabu za Kaizer Chiefs, Moroka Swallows, Black Leopards na Mpumalanga Black Aces.
Kuwamaliza ndugu zake?
Kocha huyo raia wa Malawi ana umri wa miaka 51 ameajiriwa zikiwa zimebaki siku chache tu kabla ya Yanga kuelekea nchini humo.
Yanga, mabingwa wa kihistoria Ligi Kuu Bara, watakuwa ugenini kumenyana na Silver Strikers katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ni baada ya mchezo huo, Yanga itarejea katika ardhi ya Tanzania kwa ajili ya mchezo wa marudiano utakaochezwa Oktoba 25, mwaka huu.
Mabedi pia aliwahi kuinoa timu ya taifa ya Malawi ‘The Flames’, hivyo analifahamu vizuri soka la nchi hiyo.
Kaizer Chiefs wanaijua kazi yake
Kwa mashabiki wa Kaizer Chiefs, Mabedi si jina geni. Akicheza eneo la beki wa kati, alikuwa sehemu ya kikosi cha Kaizer kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini kwa mara ya kwanza baada ya kuukosa kwa miaka 12.
Akicheza ‘pacha’ na Fabian McCarthy chini ya kocha Ted Dumitru, Kaizer walitwaa ubingwa wakiwa wamefungwa mechi tatu pekee msimu mzima.
Kabla ya kujiunga na Kaizer , Mabedi aliwahi kuitumikia Big Bullets ya Malawi kwa msimu mmoja (1997-98). Alipoondoka Kaizer mwaka 2006, vigogo wengine wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini, Moroka Swallows, walimsajili na kumtumikia kwa miaka miwili (2006–2008).
Safari yake ya ukocha
Mabedi alianzia taaluma yake ya ukocha kwa kuwanoa timu za vijana za Moroka Swallows kuanzia mwaka 2011 hadi 2015.
Baadaye, 2014–15, klabu hiyo ilimteua kuwa msaidizi wa kocha wa timu ya wakubwa, wakati huo ikinolewa na Craig Rosslee.
Msimu uliofuata, Mabedi aliondoka Swallows na kujiunga na Mpumalanga Black Aces, ambako alifanya kazi chini ya kocha mkuu, Muhsin Ertugral.
Mwaka 2016, alitumia muda mfupi akiwa msaidizi katika benchi la ufundi la timu ya taifa ya Malawi.
Alipoachana na kibarua hicho, aliajiriwa na Cape Town All Stars ya Afrika Kusini aliyoiwezesha kushika nafasi ya tisa katika msimamo wa Daraja la Kwanza nchini Afrika Kusini.
Juni, 2017, Mabedi aliajiriwa kuwa kocha msaidizi wa Kaizer Chiefs. Mwaka 2019, aliajiriwa kumsaidia kazi kocha wa Black Leopards, Lionel Soccoia, kabla ya wawili hao kutimuliwa miezi kadhaa baadaye.
Mwaka 2023, Mabedi alitangazwa kuwa kocha mkuu wa Malawi akipewa mkataba wa miaka miwili.
Uamuzi wa Mabedi kuajiriwa ulikuja baada ya Malawi kumfuta kazi Marian Mario Marinica kutokana na mfululizo wa matokeo mabaya katika mechi za kufuzu fainali za AFCON.
Kabla ya kupandishwa, Mabedi alishakuwa kocha msaidizi, ambapo aliiwezesha Malawi kufika nusu fainali ya michuano ya Cosafa. Hata hivyo, alifukuzwa kazi Oktoba, mwaka jana, baada ya Malawi kupoteza mechi tano mfululizo.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img