AMSTERDAM, Uholanzi
MFUNGAJI bora wa muda wote wa timu ya taifa ya Uholanzi, Memphis Depay, amekosekana kikosini kutokana na mkasa wa kuibiwa hati ya kusafiria.
Kwa mujibu wa Depay, ameibiwa hatia hiyo ya kusafiria akiwa Brazil, ambako anaitumikia klabu Ligi Kuu ya Corinthians.
Depay alipaswa kuungana na wenzake mazoezini juzi lakini ilishindikana baada ya kugundua kuwa asingeweza kuondoka Brazil kutokana na kukosa nyaraka hiyo.
Uholanzi chini ya kocha Ronald Koeman itashuka dimbani Alhamisi ya wiki hii kumenyana na Malta, kisha kukipiga na Finland wikiendi hii katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia za mwakani.
Akizungumzia kukosekana kwa Depay, kocha Koeman amesema: “Ni kwa bahati mbaya sana, hasa kwa Memphis na sisi pia.
“Ni sababu zilizo nje ya uwezo wetu lakini tunatarajia kuona akiunga na sisi katika kambi ya mazoezi.”
Mwezi uliopita, Depay aliingia kambani mara mbili katika mchezo dhidi ya Lithuania na kuipiku rekodi ya mkongwe Robin van Persie.
Van Persie ndiye aliyekuwa mfungaji bora wa muda wote wa Uholanzi baada ya kustaafu akiwa ameipachikia mabao 52 katika mechi 104.
Published:


