12.5 C
New York

Peru na historia ya marais wastaafu kutupwa gerezani

Published:

LIMA, Peru
KUTOKANA na sababu mbalimbali, nyingi zikihusiana na vitendo vya rushwa, marais wastaafu nchini Peru wamejikuta wakianza maisha mapya ya gerezani baada ya kutoka madarakani.
Kuthibitisha kuwa kiti cha urais kimekuwa kigumu, viongozi saba tofauti wameliongoza Taifa hilo kwa kipindi kifupi tu cha miaka saba ya hivi karibuni.
Kwa miezi miwili sasa, Rais wa zamani, Martin Vizcarra, ameendelea kusota gerezani tangu Mahakama Kuu ya nchi hiyo ilipoagiza akamatwe kutokana na tuhuma za rushwa zinazomkabili.
Vizcarra, ambaye amekana mashitaka hayo akijiita ‘muhanga wa siasa’, aliingia madarakani mwaka 2018 lakini aliondoshwa miaka miwili tu baadaye alipoanza kuchunguzwa kwa tuhuma hizo za ‘upigaji’.
Agosti 13, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Peru iliagiza Vizcarra atiwe nguvuni akishitakiwa kwa madai ya kupokea rushwa alipokuwa gavana miaka zaidi ya 10 iliyopita.
Vizcarra anashutumiwa kwa kupokea rushwa ya kiasi cha Dola za Marekani 640,000 kutoka kwa kampuni mbalimbali za ujenzi ili kuzipata kwa upendeleo tenda za serikalini.
Odebrecht ya Brazil ni miongoni mwa kampuni zilizotajwa na wakati fulani ilikiri kulipa Dola za Marekani milioni 800 kwa mataifa mbalimbali ya Amerika ili kushinda zabuni serikalini.
Kwa mujibu wa waendesha mashitaka waliopendekeza ahukumiwe kifungo cha miaka 15 gerezani, alifanya uhalifu huo kuanzia mwaka 2011 hadi 2014, wakati huo akiwa Gavana mjini Moquegua.
Baada ya agizo la Mahakama kutaka kiongozi huyo ashikiliwe kwa miezi mitano wakati huu uchunguzi ukiendelea, Vizcarra anaingia kwenye historia ya Taifa hilo kuwasotesha gerezani marais wastaafu.
Kwa miaka ya hivi karibuni, kumbukumbu zinaonesha kuwa Vizcarra anakuwa Rais mstaafu wa tano kuingia kwenye shida hiyo ya kuishi kwenye kuta za Gereza la Barbadillo, ambalo lina vyumba vidogo vitatu na limejengwa katika viwanja vya chuo cha polisi mjini Lima.
Ikumbukwe, kabla ya Vizcarra naye kupelekwa, gereza hilo lilikuwa ‘bize’ baada ya kuwapokea Alejandro Toledo, Ollanta Humala na Pedro Castillo, ambao nao walitupwa huko kwa nyakati tofauti.
Rais mstaafu wa kwanza kuonja jela alikuwa ni Alberto Fujimori, ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani mwaka 2009 kwa makosa ya ukiukwaji wa haki za binadamu wakati wa utawala wake.
Hata hivyo, Fujimori alitolewa gerezani mwaka 2023, hatua ambayo ilipingwa vikali na wananchi na kusababisha maandamano makubwa. Alifariki mwaka mmoja baadaye kutokana na ugonjwa wa saratani.
Naye Castillo aliingia gerezani kwa tuhuma za kupanga kuvunja Serikali ili aongoze nchi kwa misingi ya udikteta. Toledo aliponzwa na kosa la utakatishaji fedha alipokuwa rais mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Aidha, rushwa imeonekana kuwa ndiyo tatizo sugu katika siasa za Peru. Historia iko wazi, kwamba takribani kila rais aliyeiongoza Peru katika miaka 30 ya hivi karibuni hakuweza kukwepa tuhuma za kujihusisha na rushwa.
Hata Pedro Pablo Kuczynsk, ambaye aliiongoza Peru kwa miezi 18 tu baada ya kushinda urais mwaka 2016, alitajwa kupokea rushwa kutoka kwa kampuni zilizotaka tenda za serikali yake, ingawa hakupelekwa gerezani na badala yake alihukumiwa kifungo cha ndani.

Related articles

spot_img

Recent articles

spot_img