Na Mwandishi Wetu, Gazetini
Taarifa zinazosambazwa Jumatano, Oktoba 1, 2025 kwenye mitandao ya kijamii zikidai kutokea kwa ajali katika msafara wa mgombea urais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan mkoani Arusha ni za upotoshaji.
Gazetini Check imejiridhisha kupitia vyanzo vyake makini kuwa Dk. Samia aliwasili salama jijini Arusha akitokea Kilimanjaro pamoja na ujumbe wake wote, tayari kwa mkutano mkubwa wa kampeni uliofanyika, Alhamisi Oktoba 2, 2025, katika Viwanja vya Michezo vya Sheikh Amri Abeid.
Aidha, imebainika kuwa video na picha zinazotumika kusambaza madai hayo ni za ajali iliyotokea Februari 11, 2024, katika msafara wa aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda, mkoani Mtwara. Ajali hiyo ilihusisha magari 12 na kusababisha majeruhi na uharibifu, bila vifo.


