27.3 C
New York

Maswali tata vidonge vya uzazi wa mpango

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini
APEKSHA Shetty, mwanamke raia wa India mwenye makazi yake mjini Vienna, anasema alianza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango akiamini vingemsaidia kufurahia tendo la ndoa bila hofu ya kupata ujauzito.
Lakini, baada ya kipindi kifupi cha matumizi, Shetty akawa haingii kwenye mzunguko wa hedhi, pia akipoteza kabisa hamu ya kujamiiana na mwenza wake.
“Nilirudi kwa daktari na kumwambia sitaki maisha hayo. Mimi bado ni kijana na nataka kufanya mapenzi,” anasema katika mahojiano yake na DW.
Hata hivyo, DW inaeleza kuwa Shetty ni mmoja tu kati ya wanawake wengi wenye simulizi za namna walivyopoteza hamu ya kufanya mapenzi baada ya kutumia njia hiyo ya uzazi wa mpango.
Kwa mujibu wa DW, mahojiano yake yaliwafikia wanawake kutoka mataifa ya Afrika, Asia, Mashariki ya Kati na Ulaya, wengi wao wakisema madaktari hawakuwaambia kuwa vidonge hivyo vingeondosha hamu ya kujamiiana baada ya kuvitumia.
Mariel, raia wa Cyprus mwenye makazi yake Uholanzi, anaiambia DW kuwa alianza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango akiwa na umri wa miaka 20, wakati huo akiwa na lengo la kufurahia uhuru wa kufanya mapenzi bila hofu ya kupata ujauzito.
“Nilitaka kuwa huru zaidi. Mwanzoni, kabla ya kuanza kutumia vidonge, nilikuwa na kiwango kikubwa cha hamu ya kufanya mapenzi. Kwa kadiri nilivyokuwa natumia, nikajikuta naanza kupunguza hamu ya kushiriki,” anasema.
Lee, mwanamke mwenye umri wa miaka 40 raia wa Afrika Kusini, anasema alitumia vidonge hivyo miaka 10 iliyopita lakini aliacha miezi miwili tu baadaye, alipoanza kuona anapoteza hamu ya kufanya mapenzi.
Madai ya wanawake hao yanaonekana kuungwa mkono na majibu ya tafiti mbalimbali zilizowahi kufanywa juu ya madhara ya vidonge vya uzazi wa mpango.
Mathalan, katika utafiti uliowahi kufanywa mwaka 2013 na kuhusisha wanawake 13,000, asilimia 15 walikiri kupoteza hamu ya kufanya mapenzi mara tu walipoanza kutumia vidonge vya uzazi wa mpango.
Kama hiyo haitoshi, utafiti mwingine wa mwaka 2016 uliohusisha wanawake 340, ulibaini kuwa wengi wao walikiri kuwa matumizi ya vidonge yaliathiri hamu ya ushiriki wao katika kufanya mapenzi.
Hata hivyo, mtaalamu wa afya ya uzazi nchini India, Dkt. Tanaya Narendra, anasema bado hakuna uthibitisho wa kitaalamu kuonesha kuwa vidonge vya uzazi wa mpango vinaathiri hamu ya kufanya mapenzi.
Pia, hata kama vinahusika kwa kiasi fulani, bado wataalamu wa afya duniani kote hawakubaliani kuwa vidonge vya uzazi wa mpango ndiyo sababu pekee ya kuondosha hamu ya kufanya mapenzi kwa mwanamke.
Na badala yake, wanakubaliana kuwa kukosa hamu ya kufanya mapenzi kunaweza kusababishwa na mambo kadhaa, zikiwamo sababu za kisaikolojia au changamoto ya vichocheo (homoni).
Kwa mara ya kwanza duniani kote, Mpango wa Chakula na Dawa wa Marekani (FDA) ulitambulisha vidonge vya uzazi wa mpango mwaka 1960.
Licha ya kuwa na uhakika wa asilimia 99 katika kuzuia ujauzito, bado vidonge hivyo havijathibitika kitaalamu kuwa na uwezo wa kuzuia maambukizi ya magonjwa ya zinaa.

Related articles

Recent articles