MADRID, Hispania
KUELEKEA mchezo wao wa leo wa La Liga dhidi ya Real Oviedo, kocha wa Real Madrid, Xabi Alonso, atawakosa mastaa wake wanne.
Kwa mujibu wa taarifa, nyota watakaokuwa nje ya uwanja wakati mtanange huo ukichezwa ni Ferland Mendy, Eduardo Camavinga, Jude Bellingham na Endrick.
Mastaa hao wanaendelea na matibabu, ingawa faraja iliyopo kwa mashabiki ni taarifa za beki wa kati, Antonio Rudiger, kurejea kikosini baada ya kutumikia adhabu ya kukosa mechi dhidi ya Osasuna.
Lakini, kukosekana kwa Bellingham na Camavinga kutampa nafasi kinda wa miaka 18, Thiago Pitarch, ambaye ameonesha kiwango kizuri katika mechi alizocheza eneo la kiungo.
Akizungumzia mchezo huo, Alonso alisema: “Nina uhakika ni mechi muhimu sana kwa Oviedo na mashabiki wao. Ni nzuri kwetu pia, kuonesha tunavyoweza kucheza na kupata matokeo tukiwa ugenini.”
Wakati huo huo, wengi wanasubiri kuona kama Alonso atamtumia Rodrygo au ataendelea kumpa nafasi Brahim Diaz katika eneo la ushambuliaji.
Rodrygo raia wa Brazil, ameendelea kuhusishwa mara kwa mara na tetesi za kuondoka Santiago Bernabeu.
Nyota huyo anahusishwa zaidi na Manchester City, ingawa Liverpool na Tottenham nazo zinatajwa kuitolea macho saini yake.
Published:


