13.5 C
New York

WhatsApp kuja na huduma ya kununua vifurushi

Published:

NEW YORK, Marekani

MTANDAO wa kijamii wa WhatsApp unatarajia kuanzisha huduma mpya ya kadi za simu za kidijitali (eSIM) itakayowawezesha watumiaji kununua vifurushi vya intaneti na kuvisakinisha moja kwa moja ndani ya programu hiyo wanaposafiri nje ya nchi, hatua inayolenga kupunguza gharama za kutumia huduma za mawasiliano wanapokuwa safarini.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na tovuti ya teknolojia ya 9to5Google, huduma hiyo itawawezesha watumiaji kupata intaneti bila kutegemea huduma za gharama kubwa za roaming kutoka kwa kampuni zao za simu.

WhatsApp imesema inashirikiana na watoa huduma za eSIM pamoja na kampuni za mawasiliano zikiwemo Jio, Smart Axiata, Smart Communications na Verizon ili kuwezesha mpango huo.

Roaming ni huduma inayomwezesha mtu kutumia laini yake ya simu aliyosajiliwa katika nchi yake akiwa katika nchi nyingine, kwa kuunganishwa na mtandao wa kampuni ya mawasiliano ya nchi aliyotembelea.

Kupitia huduma hiyo, msafiri anaweza kupiga na kupokea simu, kutuma ujumbe mfupi na kutumia intaneti kwa kutumia namba yake ya kawaida. Hata hivyo, gharama za roaming, hasa matumizi ya data, zinaweza kuwa kubwa kulinganisha na vifurushi vya kawaida vya ndani ya nchi.

Tofauti na roaming, eSIM ni teknolojia ya laini ya simu ya kidijitali inayowekwa ndani ya kifaa bila kuhitaji kuingiza kadi ya kawaida ya SIM.

Kupitia huduma inayopangwa na WhatsApp, mtumiaji ataweza kununua kifurushi cha data na kusakinisha eSIM kupitia programu hiyo, huku akiendelea kutumia laini yake ya kawaida kwa huduma nyingine kulingana na uwezo wa simu yake.

Hata hivyo, huduma hiyo itakuwa ya data pekee kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa.

WhatsApp imesema huduma hiyo itaanza kutolewa katika baadhi ya nchi hivi karibuni, lakini haijabainisha tarehe rasmi ya uzinduzi, nchi zitakazonufaika awali wala bei za vifurushi.

Kampuni hiyo imesema watumiaji watajulishwa kupitia programu pindi huduma itakapopatikana katika maeneo yao, huku upatikanaji wake ukitegemea pia ushirikiano na watoa huduma za mawasiliano pamoja na simu zinazounga mkono teknolojia ya eSIM.

Related articles

Recent articles