13.5 C
New York

Pete Edochie: Kutoka uandishi wa habari hadi ustaa Nollywood

Published:

LAGOS, Nigeria

ALIFARIKI Novemba 25, 2026, akiwa na umri wa miaka 79 akiwa mjini Enugu, Kusini-Mashariki mwa Nigeria, ambako alikuwa akijiuguza maradhi ya saratani yaliyomtesa kwa muda mrefu.

Aidha, vizazi na vizazi nchini Nigeria vitaendelea kumkumbuka Pete Edochie kama mmoja ya waigizaji wa daraja la juu kwenye kiwanda cha filamu cha Nollywood.

Tangu alipochomoza kupitia tamthilia ya ‘Things Fall Apart’, Edochie hakuwahi kuwa msanii wa kawaida. Si tu ilibadilisha maisha kiuchumi, bali pia ilimpa mamilioni ya mashabiki.

Katika tamthilia hiyo iliyotokana na riwaya ya mwandishi wa vitabu mkongwe, Chinua Achebe, Edochie akitumia jina la ‘Okonkwo’ aliwavutia wengi kwa ushujaa wake kama kiongozi wa Afrika aliyepigana dhidi ya tamaduni mpya zilizoletwa na wakoloni wa Kiingereza.

KATILI ALIYEPENDWA

Kwa wapenzi wa filamu za Nigeria, kama alivyo Joy Nnamdi, wanafahamu kuwa ilikuwa ni nadra sana kumuona Edochie akicheka. Alikuwa ni mtu wa ‘scene’ za kikatili, mwenye msimamo usiyoyumbishwa na majivuno wakati mwingine.

Ungeweza kumfaidi zaidi katika sura hiyo akiwa anaigiza kama kiongozi wa kijiji, mfanyabiashara tajiri na wakati mwingine kwenye scene za kishirikana.

“Ilikuwa ngumu sana kumuona akicheka katika filamu. Alikuwa mtu mgumu kweli kweli,” anasema Nnamdi, mmoja ya mashabiki wakubwa wa Edochie nchini Nigeria.

Kwa upande wake, Sani Muazu, ambaye pia ni mfuatiliaji mzuri wa kazi za Edochie, anasema: “Kusema ukweli, wakati tunakua tulikuwa tukimuogopa. ‘Scene’ za kitakili zilimfaa sana.”

UANDISHI HADI SOKO LA FILAMU

Edochie alizaliwa Machi 7, 1947, mjini Zaria huko Kaskazini mwa Nigeria. Baada ya kuhitimu elimu ya sekondari, alisomea taaluma ya buandishi wa habari nchini Uingereza.

Aliporejea, aliajiriwa na Shirika la Habari la Eastern Nigerian Broadcasting Corporation mwaka 1967, kipindi ambacho Nigeria iliingia kwenye machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Aliwahi kuvitaja vita hivyo kama moja ya changamoto kubwa alizowahi kukutana nazo kwenye maisha yake. “Ilikuwa ngumu kupona. Njaa kali ilisababisha tuwe tunakula chochote,” alisema.

Baadaye, Edochie aliachana na tasnia ya uandishi wa habari, kisha kujitosa kwenye uigizaji ambako alidumu kwa miaka yote hadi anakutwa na umauti siku chache zilizopita.

Kwa kipindi chote alichokuwa sokoni, aliwahi kutamba na filamu nyingi nzuri, zikiwamo ‘Igodo’, ‘Rituals’ na ‘Billionaire’s Club’.

Mbali na Nigeria, alifanya kazi nchini Ghana, ambako aliigiza na wasanii wakubwa wa nchi hiyo katika filamu maarufu ya vichekesho ya ‘John and John’ ya mwaka 2017.

RAIS, MASTAA WAMLILIA

Katika salamu zake za rambirambi, Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu, amesema kifo cha Edochie ni hasara kwa soko la filamu na urithi wa utamaduni nchini humo.

Kama ilivyo kwa wengi, Rais huyo amegusia namna Edochie alivyocheza kwa kiwango bora kwenye tamthilia ya ‘Things Fall Apart’ akiigiza kwa jina la Okonkwo.

Mbali na Rais, miongoni mwa waigizaji walioshindwa kujizuia baada ya kusikia taarifa za kifo cha Edochie ni mwigizaji nguli kwa upande wa wanawake, Genevieve Nnaji.

Wakati huo huo, Patience Ozokwor, maarufu kwa jina la ‘Mama G’, ambaye ameigiza kazi nyingi na Edochie, amesema licha ya kuonekana katili kwenye filamu zake nyingi, mwigizaji huyo alikuwa mtu mwenye busara.

“Amekuwa kama baba kwenye filamu. Ningeweza kumpigia simu muda wowote na siku yoyote. Angeniambia nini cha kufanya na nini cha kuacha,” amesema Mama G.

Kwa upande wake, dairekta maarufu wa filamu, Babangida Bangis, amekiita kifo cha Edochie kuwa ni pigo kwa soko la filamu duniani, hivyo si Nigeria na Afrika pekee zilizopoteza.

“Wakati wa semina ya watengenezaji wa filamu nchini siku chache zilizopita, jina lake lilitajwa kama mfano wa ukomavu kwenye kazi, kufanya vizuri kwa muda mrefu, na weledi.

“Nafikiri kifo chake ni pigo kwa dunia, si Nigeria na wala Afrika. Sote tulikua tukimtazama na kumpenda,” amesema Babangida kuliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza [BBC].

FAMILIA YAFUNGUKA, WAWILI WAMFUATA

Nje ya kazi, Edochie alikuwa ni mtu aliyependa ukweli, kwa mujibu wa mtoto wake wa kiume, Leo Edochie, akisisitiza kuwa baba yake alikuwa shujaa na mtu aliyeiletea heshima kwenye familia.

Mtoto wa nyoka ni nyoka? Ndiyo, kati ya watoto wake sita aliowaacha Edochie, Yul na Linc wamechagua kufuata nyayo zake na sasa wako kwenye soko la filamu.

Related articles

Recent articles