13.5 C
New York

Huku kuna Wilshere, kule ni Ramsey

Published:

LONDON, Uingereza

WAKIWA makinda wa Arsenal, walicheza siku moja mechi yao ya kwanza ya timu ya wakubwa mwaka 2008, kisha wakaja kuwa viungo tegemezi katika kikosi hicho, wakati huo kocha akiwa Arsene Wenger.

Jack Wilshere alitwaa mataji mawili ya FA, wakati Aron Ramsey alibeba matatu, licha ya kwamba hakuna kati yao aliyefanikiwa kwa upande wa taji la Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wakiwa pamoja kwa miaka 10 katika eneo la kiungo la Washika Bunduki hao Kaskazini mwa Jiji la London, walicheza jumla ya mechi 101.

Kwa sasa, Wilshere na Ramsey ni makocha wa klabu za Ligi Daraja la Pili nchini England [League One], kila mmoja akiipambania timu yake kupanda Ligi Daraja la Kwanza [Championship].

Wilshere anainoa Luton Town, klabu iliyoibua kipaji chake na kisha kumuuza Arsenal akiwa kinda, wakati Ramsey analiongoza benchi la ufundi la Oxford United na timu hizo zilikutana Jumamosi ya jana Novemba 28, 2026.

Baada ya kustaafu kucheza soka mwaka 2022, Wilshere alianza kuinoa U-18 ya Arsenal, klabu iliyomkuza kupitia ‘academy’ hadi kuwa mchezaji muhimu wa kikosi cha kwanza, kabla ya kwenda Norwich City kama kocha mkuu msimu wa 2024-25.

Ramsey alipostaafu kucheza soka alianza kupata uzoefu wa ukocha akiwa na vijana wa U-18 ya Cardiff City, klabu iliyoibua kipaji chake akiwa mdogo.

Jana haikuwa mara ya kwanza kwa Wilshere na Ramsey kukutana wakiwa makocha. Mara ya kwanza ilikuwa Mei, 2025, ambapo Norwich ya Wilshere iliifunga Cardiff mabao 4-2.

Wawili hao wanaungana na wakongwe wenzao wa Arsenal waliogeukia taaluma ya ukocha tangu walipostaafu kucheza soka, wakiwamo Mikel Arteta, Patrick Vieira, Thierry Henry, Ashley Cole, Robin van Persie, Kolo Toure na Cesc Fabregas.

Related articles

Recent articles