MONROVIA, Liberia
LIBERIA imepokea wahamiaji 25 waliofukuzwa kutoka Marekani, wakiwamo wanawake wawili, hatua inayotokana na sera kali za uhamiaji zinazoendelea kutekelezwa na Rais Donald Trump.
Taarifa kutoka Tume ya Urejeshaji, Makazi na Ujumuishaji wa Wahamiaji ya Liberia (LRRRC), iliyotolewa kupitia Shirika la Habari la AFP, zinasema kundi hilo lilifika nchini humo Ijumaa saa 3:35 usiku kwa saa za eneo hilo.
Kwa mujibu wa mwakilishi wa Tume hiyo, wengi wa wahamiaji hao wanatoka Amerika Kusini, ingawa hakutoa maelezo zaidi kuhusu mataifa yao.
Liberia ni miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyokubali kupokea wahamiaji wanaofukuzwa kutoka Marekani. Serikali hiyo imetangaza kuwa iko tayari kupokea hadi watu 1,200 kutoka mataifa mengine ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Mataifa mengine yaliyokubali kushiriki mpango huo ni Sierra Leone, Guinea ya Ikweta, Ghana, Rwanda, Sudan Kusini, Cameroon, Eswatini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Baadhi ya makubaliano hayo yanaripotiwa kuhusisha msaada wa kifedha au vifaa kutoka Marekani. Hata hivyo, Serikali ya Liberia imewahi kueleza kuwa haikudai wala kupokea fidia au ahadi ya zawadi yoyote ili kushiriki katika mpango huo.
Pamoja na kauli hiyo, gazeti la The New York Times liliripoti kuwa Marekani ilifanya malipo ya dola milioni tano kwa Liberia, kwa mujibu wa nyaraka zilizoidhinishwa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kufuatia ahadi ya Liberia ya kuzingatia kupokea wahamiaji hao.
Kundi hilo ni miongoni mwa wahamiaji wa hivi karibuni kuwasili Liberia katika kipindi cha miezi minne iliyopita, tangu Trump aanzishe hatua kali za kudhibiti uhamiaji.
Wakati huohuo, Gavana wa Jimbo la Washington, Bob Ferguson, amekosoa vikali operesheni za maafisa wa uhamiaji wa Marekani (ICE), akizitaja kuwa zimekiuka mipaka ya mamlaka yao baada ya kuwakamata watu wawili katika uwanja wa ndege wa Seattle.
Ferguson alisema maafisa hao walionyesha tabia isiyokubalika baada ya kuwakamata watu hao wakiwa katika daraja la kuingia ndani ya ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Seattle-Tacoma Jumamosi.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha watu wawili wakikamatwa na wanaume waliovaa barakoa. ICE ilithibitisha kuwakamata watu hao, ikieleza kuwa walikuwa wamezidisha muda wa vibali vyao vya kuishi nchini humo.
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa X, Ferguson alisema amekerwa na kitendo cha maafisa hao waliovaa barakoa kuwakamata watu bila kujitambulisha, hali aliyodai ilisababisha taharuki katika jamii.
ICE ilieleza kuwa operesheni hiyo ililenga kumkamata Ricardo Larrondo Mendoza, raia wa Mexico aliyedaiwa kuzidisha muda wa visa yake. Mtu wa pili, Sofia Mejia, pia raia wa Mexico, alikamatwa na shirika hilo likidai alimshambulia afisa wa serikali kwa kumrushia kahawa ya moto.
Kampuni ya ndege ya Alaska Airlines ilisema ina wasiwasi kuhusu tukio hilo, huku ikisisitiza kuwa inawajibika kufuata sheria inaposhirikiana na vyombo vya usalama, lakini haihusiki kupanga au kuratibu operesheni za uhamiaji.
Tukio hilo limeibuka wakati Serikali ya Trump ikiendelea na operesheni za kuwabaini na kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali halali, licha ya kukabiliwa na ukosoaji kutoka kwa baadhi ya viongozi na wananchi wa Marekani.


