KAMPALA, Uganda
KWA kipindi cha miezi 15 ya hivi karibuni, majenerali wa jeshi wasiopungua 10 wamekamatwa na kushikiliwa gerezani. Hiyo ndiyo sura ya jeshi la Uganda chini ya Mkuu wake, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni.
Jenerali Muhoozi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi mwanzoni mwa mwaka 2024. Kabla ya hapo, alikuwa akiiiongoza SFC, kitengo maalumu kinachompa ulinzi baba yake, Rais Museveni. Kwa muundo wa jeshi la Uganda, anaripoti kwa Rais Museveni, hivyo kuwa na uhuru na nguvu kubwa ya ndani ya taasisi hiyo.
MAJENERALI WA JESHI KIKAANGONI
Mathalan, kushikiliwa kwa Luteni Jenerali Peter Elwelu kumezua gumzo kubwa. Alikamatwa Novemba 2, 2026, kwa madai kuwa alisuka mpango wa kutibua amani katika Mkoa wa Teso.
Wakati huo huo, Elwelu ni mmoja tu kati ya majenerali na viongozi waaandamizi wengine wa jeshi walioshikiliwa tangu Aprili, 2025, kwa mujibu wa uchunguzi wa Gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda. Miongoni mwao wapo viongozi watatu wa zamani wa usalama wa taifa.
Baada ya kukamatwa, Jenerali Muhoozi alitumia mitandao ya kijamii kumwita msaliti, achilia mbali hatua kubwa zaidi ya kumvua hadhi ya nyota tatu aliyokuwa katika utumishi wake jeshini.
Haikuishi kwake tu. Jenerali Muhoozi mwenye umri wa miaka 52, alitumia ukurasa wake wa mtandao wa kijanii wa X kutangaza kuwa mamlaka zinawashikilia wanajeshi zaidi ya 20 waliokuwa na Elwelu.
Aidha, Jenerali Muhoozi aliyafanya yote hayo kinyume cha sheria za jeshi, ambazo haziruhusu kiongozi mwandamizi kuvuliwa nyota kupitia mitandao ya kijamii.
Agosti, 2025, mamlaka zilimkamata aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Taifa, Meja Jenerali James Birungi, kwa tuhuma za mbalimbali, ikiwamo uhaini, ugaidi na rushwa.
Alishitakiwa na mahakama ya kijeshi, kabla ya kuachiwa baada ya Jenerali Muhoozi kusema amemsamehe. Ni mazingira hayo hayo yalitokea kwa Brigedia Jenerali Charles Bakahumura.
Septemba, 2026, alikamatwa kiongozi mwingine wa zamani wa Usalama wa Taifa, Meja Jenerali Abel Kandiho, ambaye bado anashikiliwa, kwa mujibu wa ripoti ya Daily Monitor.
UPINZANI WA KISIASA JESHINI
Kamatakamata hiyo ya majenerali wa jeshi inakuja wakati huu Jenerali Muhoozi akihusishwa na mpango wa kumrithi baba yake, Rais Museveni, aliyeiongoza Uganda kwa miaka zaidi ya 40.
Wakati wengine wakimpongeza kwa madai kwamba anawashughulikia viongozi wa jeshi wanaojihusisha na rushwa, mtazamo tofauti ni kwamba wanaoshughulikiwa ni wale wanaopinga mwenendo wake na wasiotaka kumuunga mkono kwenye mBio zake za kutaka urais.
Kwa upande wake, Dk. Gerald Bareebe, mzaliwa wa Uganda na mchambuzi wa siasa katika Chuo Kikuu cha York nchini Canada, anauona uhusiano mkubwa kati ya kamatakamata ya majenerali na mkakati wa kusaka urais alionao Jenerali Muhoozi.
“Maofisa waandamizi [wa jeshi] wasiouunga mkono mpango wake wamekuwa wakikamatwa, wakishikiliwa na kufunguliwa mashitaka ya rushwa na uhaini,” amesema Dk. Bareebe akihojiwa na BBC.
Zipo taarifa, ambazo hata hivyo zimekanushwa na Serikali, kwamba baadhi ya maofisa wameachiwa baada ya kuingia makubaliano ya kumuunga mkono Jenerali Muhoozi katika harakati zake za kutaka urais.
Lakini, baadhi ya wasiovutiwa naye ndani ya jeshi hawakubaliani na mtindo wake wa kutumia mitandao ya kijamii, hasa X [zamani Twitter], badala ya njia rasmi za mawasiliano ndani ya chombo hicho.
TISHIO KWA MAKAMU WA RAIS
Usiku wa Novemba 9, 2026, Jenerali Muhoozi alithibitisha jeuri yake kwa kutishia kumng’oa madarakani na kumkamata Makamu wa Rais, Jessica Alupo. Tishio hilo lilikwenda sambamba na kusema angeweza kuchukua nafasi hiyo ya Makamu wa Rais.
“Yeyote aliye kwenye nafasi hiyo, anapaswa kujiandaa kuikabidhi hivi karibuni,” aliandika kupitia X, ingawa alifuta ujumbe huo hapo baadaye.
Jenerali Muhoozi alikosoa utiifu wa Alupo kwa Serikali ya Rais Museveni, akisisitiza kuwa Uganda itaongozwa kijeshi endapo atakuwa kwenye nafasi hiyo ya Makamu wa Rais. Alupo amebaki kwenye nafasi hiyo na hajatoka hadharani kujibu.
CHAMA TAWALA KINAMPINGA?
Hata hivyo, wakati huu Jenerali Muhoozi akionekana kujiandaa kuwa Rais mpya wa Uganda, zipo taarifa kuwa Chama tawala, National Resistance Movement (NRM), hakivutiwi na hakimuungi mkono.
Ikaelezwa kwamba kilifanyika kikao Kizito cha viongozi wa NRM lakini kilimalizika bila kufikia mwafaka juu ya kumuunga mkono; wapo waliokubali, lakini wengine walisema hafai kuwa kiongozi wa umma.
Na badala yake, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uganda, baadhi ya viongozi wa NRM wanavutiwa zaidi na mtoto mwingine wa Rais Museveni, Jenerali Salim Saleh, kurithi kiti cha baba yake.
Lakini, NRM imekanusha taarifa hizo kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Richard Todwong Awany, aliyedai kuwa huu si wakati mwafaka kujadili nani anapaswa kugombea kiti cha urais.
UCHAGUZI MKUU MWAKA 2031
Rais Museveni mwenye umri wa miaka 82, amekuwa kiongozi wa Uganda tangu alivyoingia madarakani kwa vita vya msituni mwaka 1986. Mapema mwaka huu, aliapishwa na kuanza muhula wake wa saba. Jenerali Muhoozi amekuwa akitajwa kuwa ndiye anayeandaliwa kuwa rais ajaye kupitia Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2031.
Wakati Jenerali Muhoozi akiendeleza kampeni yake, hali ni mbaya kwa upande wa wanasiasa wa upinzani. Mkongwe Kizza Besigye anasota gerezani kwa mashitaka ya uhaini.
Bobi Wine, ambaye alishika nafasi ya pili nyuma ya Rais Museveni katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, amelazimika kuondoka Uganda akihofia usalama wake, na sasa anaishi Marekani baada ya kutishiwa maisha na Jenerali Muhoozi.


