7.5 C
New York

Shule ‘chafu’ kuzuiwa udahili wa wanafunzi

Published:

Na Editha William, Gazetini – KAGERA

SHULE za bweni mkoani Kagera zitakazoshindwa kutekeleza maelekezo ya usafi wa mazingira na kuangamiza wadudu waharibifu hazitaruhusiwa kupokea wanafunzi katika mwaka ujao wa masomo [2026-27].

Huku ukaguzi maalumu ukitarajiwa kuanza Desemba 21, 2026, hadi Januari 15, 2027, hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Ofisi ya Afya Mkoa wa Kagera kuhakikisha shule za bweni zinazingatia viwango bora vya afya na usalama, hususan katika maeneo ya kulala, maghala ya chakula na vyanzo vya maji vinavyotumiwa na wanafunzi.

Katika kutekeleza mkakati huo, maafisa afya wa Wilaya wameagizwa kukagua maghala ya chakula na kuhakikisha vyakula vilivyoharibiwa na wadudu vinaondolewa, huku vyakula vinavyobaki vikihifadhiwa katika mazingira salama.

Akizungumzia hilo, Afisa Afya Mkoa wa Kagera, Yasin Mwinori, amesema: “Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira safi na salama wanapokuwa shuleni. Wamiliki wa shule wanatakiwa kutekeleza maelekezo yote ndani ya muda uliowekwa.”

Aidha, shule zimetakiwa kusafisha visima na mifereji ya kukusanyia maji ya mvua, pamoja na kutumia dawa za klorini kuhakikisha yanakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.

Ukaguzi huo utafanywa kwa ushirikiano kati ya Idara za Afya na Elimu baada ya maafisa afya wa halmashauri zote nane kuwasilisha taarifa ifikapo Desemba 20, 2026, kuhusu shule zilizotekeleza agizo la kufanya usafi na kupuliza dawa za kuangamiza wadudu waharibifu.

Related articles

Recent articles