7.5 C
New York

Dk. Mwinyi: Vijana changamkieni fursa sayansi ya anga

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini – ZANZIBAR

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu kwa vijana, kufuatia kufunguliwa kwa Kituo cha Elimu ya Anga cha Zanzibar Astronomy and Space Society (ZASS), kilichopo Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja.

Akizungumza leo Novemba 14, 2026, wakati wa kufungua kituo hicho na kuzindua Mradi wa Zanzibar Observatory and Planetarium, Dk. Mwinyi amesema uwekezaji huo utawapa vijana fursa ya kujifunza sayansi ya anga kwa vitendo, kufanya tafiti, kukuza vipaji na kubuni teknolojia zitakazosaidia kutatua changamoto za jamii.

Amezielekeza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali pamoja na Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu kushirikiana na ZASS kuhakikisha elimu ya sayansi ya anga inawafikia wanafunzi wengi zaidi.

Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa kituo maalumu cha kuhifadhi historia ya Zanzibar kupitia Mradi wa Mercury wa NASA, huku akikubali kuwa mlezi wa ZASS ili kuunga mkono juhudi za kukuza sayansi nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa ZASS, Amina Ahmad, amesema kituo hicho kitakuwa na eneo la uchunguzi wa anga, ukumbi wa kidijitali wa maonesho na programu za elimu zitakazoiweka Zanzibar katika nafasi mpya ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Katika hafla hiyo, Dk. Mwinyi alitembelea mabanda ya wanafunzi na kujionea bunifu mbalimbali za kisayansi kabla ya kuzindua rasmi kituo hicho.

Related articles

Recent articles