UYO, Nigeria
TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeambulia kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa wenyeji wao, Super Eagles, katika mchezo wa kufuzu fainali za AFCON 2027 uliochezwa leo Novemba 13, 2026, nchini Nigeria.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabio, Eagles walipata mabao mawili kutoka kwa mchezaji aliyetokea benchi, Tolu Arokodare, huku jingine likifungwa na Alhassan Yusuf.
Bao pekee la Stars katika mchezo huo lilifungwa na Alphonce Msanga katika dakika ya 32 akitumia ‘asisti’ ya Novatus Miroshi. Bao hilo lilifanya mchezo uwe sare ya bao 1-1, kabla ya Nigeria kuongeza mawili.
Ni baada ya matokeo hayo sasa, Eagles watafunga safari hadi Tanzania kwa mchezo wa marudiano unaotarajiwa kuchezwa Novemba 17, 2026.
KENYA YAITIKISA BAFANA BAFANA
Kikosi cha Harambee Stars kikiwa ugenini kimepata sare ya mabao 2-2 mbele ya Afrika Kusini ‘Bafana Bafana’ katika mchezo mwingine wa leo uliochezwa kwenye Uwanja wa Orlando mjini Soweto.
Wenyeji wa mchezo, Bafana Bafana, walitangulia kwa bao la dakika ya 9 baada ya nyota wa Kenya, Amos Wanjala, kujifunga katika hekaheka za kuokoa.
Harambee Stars walisawazisha bao hilo dakika chache kabla ya mapumziko kupitia kwa Michael Olunga aliyefunga kwa mkwaju wa penalti baada ya mchezaji wa Bafana Bafana ‘kuunawa’ mpira ndani ya boksi.
Katika dakika ya 77 ya mchezo huo, Relebohile Mofokeng aliifungia Bafana Bafana bao la pili, kabla ya Ryan Ogam aliyetokea benchi kuisawazishia Harambee Stars na kuipa pointi moja ya ugenini.
YALIYOJIRI VIWANJA VINGINE
Mchezo mwingine wa kufuzu AFCON 2027 uliochezwa jana uliishuhudia Guinea-Bissau ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na Madagascar.
Siku hiyo hiyo, Senegal waliondoka na ushindi mnono wa mabao 4-1 dhidi ya Sudan, wakati Ghana waliifunga Somalia mabao 2-0, huku DR Congo, Ivory Coast, Benin na Cameroon nazo zikipata ushindi katika mechi zake.


