Na mwandishi Wetu, Gzetini – SHINYANGA
KATIKA kipindi cha miezi sita kuanzia Aprili hadi Septemba, 2026, Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Shinyanga imeokoa Shilingi 236,069,957 kutokana na udhibiti wa makusanyo ya mapato, pamoja na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 13, 2026, na Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoani Shinyanga, Mwamba Massanja, wakati akitoa taarifa ya robo mbili za mwaka 2026, huku akihimizi wananchi kushirikiana na Taasisi hiyo kuzuia na kupambana na rushwa.
Amesema Shilingi 75,500,500 zimeokolewa kupitia ufuatiliaji kwenye ukusanyaji mapato kwa njia ya mashine za kielektroniki katika mnada wa Old Shinyanga, ambapo mawakala walibaki na fedha hizo, badala ya kuzipeleka benki kwa wakati.
“Shilingi 47,877,360 zilitokana na ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za ununuzi wa pamba msimu wa mwaka 2025-26 wilayani Kishapu. Makampuni yalikabidhi fedha kwa vyama vya msingi (AMCOS) kwa ajili ya manunuzi ya pamba kwa wakulima lakini kulikuwa na sintofahamu ya malipo ya wakulima na baada ya ufuatiliaji wakulima walilipwa,” ameongeza Massanja.
Mbali na hilo ameongeza kuwa, “Sh. 35,129,844.63 zimeokolewa kutoka kwa wadaiwa sugu wa ushuru wa huduma (Service Levy) Kahama ambao walikwepa kulipa kwa muda mrefu” amesema Massanja.
Katika suala la kuzuia rushwa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kumi yenye thamani ya Sh. 27.9 billioni umefanyika katika miradi ya afya, elimu, barabara, huduma za jamii na utawala.
Mbali na hilo, TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia makundi mbalimbali, zikiwamo klabu za kupinga rushwa, semina, mikutano, maonyesho, pamoja na vyombo vya habari.
Aidha, Massanja ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Shinyanga kushirikiana kikamilifu na Takukuru katika kuzuia rushwa kwenye suala zima la utekelezeji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma za kijamii na ujenzi wa taifa.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo mkazi wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga Japhet Maige amesema kuwa, “Kazi inayofanywa na Takukuru ni nzuri kwani inaonyeshwa ubadhilifu wa fedha za umma unaofanywa na baadhi ya watumishi wasio waadilifu kwenye kazi, pia tunaomba waongeze kasi zaidi katika ufuatiliaji na kuifikiwa miradi ya vijijini” amesema.


