Na mwandishi wetu, Gazetini
DONALD Trump anaweza kuwa Rais ‘mtata’ zaidi kuwahi kutokea katika historia ya Marekani kwa miaka ya hivi karibuni. Kauli na vitendo vyake vimekuwa gumzo tangu alipoingia Ikulu na hii ni awamu yake ya pili kuiongoza nchi hiyo.
Nje ya siasa, Rais Trump anatokea familia ya kitajiri. Alianza kuongoza biashara za familia mwaka 1971 akiwa mtoto wa nne kwenye familia ya tajiri wa biashara ya kujenga na kupangisha majengo, Fred Trump.
Licha ya utajiri wa familia yao, Trump alianzia katika kazi za kipato cha chini kwenye kampuni ya baba yake baada ya kutoka chuo cha kijeshi alikopelekwa kutokana na utukutu wake akiwa kijana mdogo wa miaka 13.
Alipohitimu masomo ya elimu ya juu ngazi ya Shahada katika Chuo Kikuu cha Wharton, Trump alianza kumsaidia baba yake kwenye biashara ya kuuza na kupangisha majengo.
Alipata nafasi hiyo baada ya kaka yake, Fred, kuamua kuwa rubani, kabla ya kufariki kwa ulevi wa pombe akiwa na umri wa miaka 43. Trump alisimamia biashara hizo hadi mzee wake alipofariki mwaka 1999.
Kwa kiasi kikubwa, aliweza kuboresha mwonekano wa biashara ya familia, akiongeza ubunifu wa kuanzisha kumbi za starehe [casino], viwanja wa gofu na hoteli za kifahari ndani na nje ya Marekani.
Akihojiwa mwaka 1980, Trump akiwa na umri wa miaka 34 wakati huo alisema watu wenye uwezo mkubwa hukimbilia biashara na si siasa.
Hata hivyo, ilipofika mwaka 1987, alianza kuonesha tamaa ya kuwania kiti cha urais lakini mwaka 2015 ndipo Trump alipotangaza nia ya kugombea urais.
Akitumia kaulimbiu ya ‘Make America Great Again’, Trump aliweza kuwapiku wapinzani wake ndani ya Chama chake cha Repulican na hatimaye kupitishwa kugombea urais dhidi ya Hillary Clinton wa Democrat. Hatimaye, akaandika historia ya kuwa rais wa 45 wa Marekani na kuapishwa Januari 20, 2017.
Kwa sasa, Trump ni mume wa mshindi wa zamani wa taji la urembo nchini Slovenia, Melania Knauss. Walifunga ndoa mwaka 2005 na wamebahatika kupata mtoto mmoja, Barron William Trump [18].
Kabla ya kuangukia kwa Melania, aliwahi kuwa na mahusiano na wanawake tofauti, akiwamo mke wake wa kwanza, Ivana Zelnickova.
Huyo ni mwanamtindo wa zamani wa Jamhuri ya Czech na kabla ya ndoa yao kuvunjika mwaka 1990 ilibahatika kupata watoto watatu [Donald Jr, Ivanka na Eric].
Alipoachana na Zelnickova, Trump alimuoa mwigizaji maarufu wa filamu, Marla Maples, mwaka 1993. Walipata mtoto mmoja, Tiffany, kisha wakaachana mwaka 1999.


