Na mwandishi wetu, Gazetini
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limetoa onyo kwa watu wanaodaiwa kupanga kuhamasisha vurugu na uvunjifu wa amani jijini humo wakati wa kutolewa kwa hukumu ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, inayotarajiwa Novemba 6, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Novemba 3, 2026, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum, Jumanne Muliro, amesema Jeshi hilo limepokea taarifa kuhusu kuwepo kwa kundi la watu wanaodaiwa kuwa na mipango ya kufanya fujo, vurugu au hujuma siku hiyo.

“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kwa kundi la watu waliopanga kuja Dar es Salaam kuhamasisha vurugu siku ya Ijumaa wakati wa hukumu ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu. Jeshi la Polisi litazuia na kushughulika na mtu yeyote au kikundi kitakachobainika kuwa katika mipango hiyo ya fujo,” alisema Muliro.
Alisisitiza kuwa Jeshi hilo halitavumilia vitendo vya vurugu au hujuma za aina yoyote, akieleza kuwa litachukua hatua za haraka na za kisheria dhidi ya watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Aidha, aliwataka wananchi kuzingatia utaratibu uliowekwa na Mahakama katika kufuatilia mashauri mbalimbali na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa jamii.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa litaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria ili kuhakikisha usalama na amani vinadumishwa wakati wa tukio hilo.


