Na Hassan Mwasha, Gazetini
HIVI karibuni, Katibu wa Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Chacha, alitoa kauli iliyoibua mjadala mzito na wengine wakiitafsiri kuwa ni mwendelezo wa tabia za baadhi ya viongozi kujisahau, kutafuta ‘kiki’ au kujikomba kwa wakubwa zao [uchawa].
Katika moja ya mikutano ya hadhara, Chacha alisema vyombo vyote vya ulinzi na usalama viko chini ya CCM, akifahamu wazi kuwa kauli yake hiyo inakinzana na kile kinachoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yam waka 1977.
Baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza mwaka 1992, Katiba iliweka wazi kuwa vyombo vya dola si mali ya chama kimoja [kama ilivyokuwa awali], lengo likiwa ni kuleta usawa katika uwanja wa siasa za ushindani.
Tujiulize; Chacha halijui hilo? Kama hajui, anawezaje kuwa kiongozi wa ngazi za juu katika Chama kikongwe kama CCM, ikiwa haijui hata Katiba anayojinasibu kuilinda? Na kama anajua, kwanini aliona ni sahihi kwake kupingana na kilichoandikwa kwenye Katiba? Ikiwa yeye ni kiongozi asiyeheshimu Katiba, vipi kwa anaowaongoza?
Pili, kwa miaka mingi, yamekuwapo malalamiko ya hapa na pale kutoka kwa vyama vya upinzani, kwamba vyombo vya dola nchini vimekuwa vikiibeba CCM, hivyo ‘kuua’ ushindani wa kisiasa. Ni mara nyingi tu wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakiibua madai ya polisi na wakati mwingine jeshi la wananchi kuingia kwenye uwanja wa siasa kwa lengo la kuisaidia CCM.
Mara zote hizo, polisi na jeshi wamekuwa wakikanusha madai hayo. CCM nao, kwa nyakati tofauti, wamejitahidi kujiweka kando na tuhuma hizo. Hivyo, wananchi hawakuwahi kukubaliana na madai hayo ya upinzani.
Je, kwa kauli ya sasa ya ndugu Chacha, ni wakati sahihi kuamini kuwa CCM na vyombo hivyo vya ulinzi na usalama ni ‘pete na kidole’? Kama sivyo, Chacha ametoa wapi uhusiano huo? Ametoa wapi utubutu wa kuvisingizia vyombo vya dola?
Bila shaka, kama amevisingizia, vyombo hivyo vilipaswa kumkamata kwani si tu ameviingiza kwenye ‘uadui’ na wananchi wasio wafuasi wa CCM, bali pia ameviondoshea kuaminika kwake. Kwa ufupi, amechafua taswira ya vyombo hivyo mbele ya macho ya umma.
Tatu, CCM imebaki kimya hata baada ya kusikia ikisingiziwa kuwa inamiliki vyombo vya ulinzi na usalama. Ukimya huo una maana moja tu, kwamba Chacha yuko sahihi.
Ndiyo, kama ni kinyume chake, isingechukua saa 24 kabla ya kusikia tamko la Umoja wa Vijana wa Chama [UVCCM] kupingana na kauli za Chacha. Wako kimya, licha ya historia yao nzuri ya kumshughulikia kila waliyeamini ni adui, bila kujali ukubwa wake ndani ya Chama.
Kwa nyakati tofauti, Joseph Sinde Warioba, Edward Lowassa, Fredrick Sumaye, Humphrey Polepole na Dkt. Emmanuel Nchimbi aliyejiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais hivi karibuni waliwahi kujeruhiwa na makucha ya vijana wa Lumumba.
Sasa tujiulize; ukimya wao kwa ndugu Chacha ni kwamba wamekubali Chama chao kusingiziwa kuwa kinamiliki polisi na jeshi? Kinyume cha hapo, wanakubaliana na Chacha kwamba vyombo hivyo ni mali ya CCM.
Kwamba Chama, ambacho kimejinasibu kwa miaka mingi kuwa ni chaguo la wananchi walio wengi, kimekuwa kikiinajisi Katiba inayotaka vyombo vya usalama kutokuwa sehemu ya siasa. Kwa ukongwe, ukomavu na weledi wa CCM, hutegemei kuona ikikubali kuwa mfano wa taasisi zisizoheshimu Katiba. Hivyo, inapaswa kujitenga na Chacha na kisha kumchukulia hatua kwa masilahi mapana ya Chama.


