18.6 C
New York

Rick Ross aliiba jina la muuzaji ‘unga’, aliacha soka kisa Hip Hop

Published:

LOS ANGELES, Marekani

KAMA utataja wasanii wa Hip hop wakubwa nchini Marekani na duniani kwa ujumla, basi hutoacha kulitaja jina la William Leonard Roberts II, maarufu kwa jina la Rick Ross.

Mbali na tuzo nyingi alizobeba, Ross ni miongoni mwa wanamuziki matajiri nchini Marekani, akifahamika kwa staili yake ya kuanika maisha ya aina, hasa magari na mijengo anayomiliki.

JINA LA MUUZAJI ‘UNGA’

Mwanzoni mwa safari yake ya muziki, rapa huyo aliyezaliwa Januari 28, 1976 na kukulia katika mitaa ya Florida hakuwa akitumia jina la Rick Ross na badala yake alijiita Teflon Da Don.

Katika miaka ya 2000, ndipo alipoanza kujiita Rick Ross, jina la aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa dawa za kulevya. Baadaye, mfanyabiashara huyo alijaribu kufungua kesi ya kumshitaki rapa huyo kwa madai ya kutumia jina lake lakini hakuweza kumtia hatiani.

SOKA NA KUACHA CHUO

Akiwa mdogo, Ross alipenda kucheza soka. Ni mchezo aliomudu vizuri kiasi cha kupata ufadhili wa masomo katika Chuo Kikuu cha Jimbo la Albany (ASU) huko Georgia. Hata hivyo, hakumaliza masomo na badala yake akarejea Florida kuendelea na Maisha mengine. Kuanzia mwaka 1995 hadi 1997, alikuwa mfanyakazi katika gereza Florida.

Ross alianza kujihusisha na muziki, kabla ya kusainiwa na lebo ndogo ya mtaani iitwayo Suave House Records. Ni hadi ilipofika mwaka 2006, ndipo alipoachia ngoma ‘Hustlin’ iliyompa jina na nafasi ya kusainiwa na Slip-n-Slide Records iliyokuwa chini ya Def Jam.

Chini ya lebo hiyo ndipo alipokua zaidi, hasa baada ya albamu yake ya kwanza iitwayo ‘Port of Miami’ kushika namba moja kwenye chati za Billboard 200.

AANZISHA LEBO YAKE

Baada ya miaka miwili ya mafanikio akiwa Def Jam Recordings, ‘Rozay’ mwenye umri wa miaka 50 aliondoka na kuanzisha lebo yake ya Maybach Music Group (MMG) ambayo baaaye iliwasaini Meek Mill, Wale, French Montana na Omarion.

Chini ya lebo yake, ‘The Boss’ aliweza kuachia albamu zingine tano, ambazo ni ‘Trilla’ (2008), ‘Deeper Than Rap’ (2009), ‘Teflon Don’ (2010), ‘God Forgives, I Don’t’ (2012) na ‘Mastermind’ (2014).

MMG kwa kushirikiana na Def Jam na baadaye Epic Records, Ross aliachia albamu zingine za ‘Hood Billionaire’ (2014), ‘Black Market’ (2015), ‘Rather You Than Me’ (2017), ‘Port of Miami 2’ (2019) na ‘Richer Than I Ever Been’ (2021).

UTAJIRI WA KUTISHA

Kwa mujibu wa jarida la Forbes, Ross ni miongoni mwa mastaa wa muziki wenye mkwanja mrefu duniani. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya Forbes, jamaa ana utajiri unaofikia Dola za Marekani milioni 150. Ni kawaida yake kuposti nyumba, magari na vitu vingine vya gharama anavyomiliki.

Forbes inaeleza pia, nyumba anazomiliki zina thamani ya zaidi ya Dola milioni 100 na wakati huo huo thamani ya jumla kwa magari yake ni Zaidi ya Dola milioni 3.5.

BIFU NA 50 CENT

Kama kuna alama kubwa kwenye maisha yake ya muziki, ni pamoja na ugomvi wake na rapa mwenzake, 50 Cent. Haijawahi kufahamika sababu ya vita vyao lakini walikuwa ‘chui na paka’ kuanzia mwaka 2009. Kila mmoja aliachia ngoma za ‘kum-diss’ mwenzake, kabla ya kuamua kuelewana na sasa ni marafiki.

Related articles

Recent articles