Na Hassan Mwasha, Gazetini
MAMBO magumu! Kagera Sugar na Pamba Jiji ndizo timu mbili pekee ambazo hadi kufikia hatua hii hazibahatika kupata ushindi, licha ya kushuka dimbani mara sita msimu huu wa Ligi Kuu Bara [2026-27].
Kwa mujibu wa kile kinachoonekana kwenye msimamo wa Ligi, timu zote ziko kwenye hatari ya kushuka daraja kwani Kagera Sugar ya mkoani Kagera, inashika nafasi ya 15, juu ya Pamba Jiji inayoburuza mkia.
Walau Kagera wao wameambulia sare mbili na kufungwa mechi nne, hivyo wamekusanya jumla ya pointi mbili, wakati Pamba wana sare moja na kupotea mechi zao tano za Ligi.
Aidha, bado hali ni mbaya pia kwa Fountain Gate na TRA United kwani ndizo timu pekee zilizoshinda mara moja, licha ya kwamba tayari zina mechi sita zilizocheza.
Je, timu hizo zilizo kwenye ‘ICU’ ya Ligi Kuu Bara zitaamka usingizini baada ya mapumziko ya sasa ya kupisha mechi za kimataifa zilizo kwenye kalenda ya FIFA [Shirikisho la Soka la Kimataifa]?


