Na Hassan Mwasha, Gazetini
KWA upande wa matokeo, ni ngumu kukubaliana na wanaomkosoa. Ameshinda mechi zote sita kwenye Ligi Kuu msimu huu wa 2026-27. Hajafungwa katika michezo miwili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Alitoa sare ya ugenini dhidi ya Gaborone United, kisha akaifunga 2-1 jijini Dar es Salaam.
Hivyo, kama ni upande wa takwimu za matokeo, unaweza usione tatizo na utasimama na kocha huyo wa Yanga raia wa Afrika Kusini, Manqoba Mngqithi, na kuwapinga kwa nguvu zote wale wanaomkosoa. Utamuona ni kocha aliye salama kwenye kibarua chake.
Hata hivyo, shida waliyonao Wanayanga iko kwenye maeneo mawili. Mosi, licha ya kushinda, hawaridhishwi na kiwango kinachooneshwa na timu yao ndani ya uwanja. Wanataka ushindi unaotokana na soka la kuvutia.
Staili ya uchezaji wa timu kwa sasa inawaweka ‘roho juu’ katika kila dakika ya mchezo, hata pale timu yao inapokuwa inaongoza. Hilo lilionekana wazi katika mechi mbili za ushindani zilizopita [dhidi ya Gaborone na Geita Gold]. Yanga ilishinda lakini mashabiki wake walikiona cha moto.
Manqoba amekuwa muumini wa kujilinda baada tu ya kupata bao na hiyo inakinzana na utamaduni wa Yanga kwa miaka ya hivi karibuni, ambapo imezoea kushinda ikiwa inatawala sehemu kubwa ya mchezo. Wanakufunga na wanakupigia mpira.
Kwa kocha waliye naye sasa, wanapata ushindi wakiwa wamezishikilia roho zao mkononi. Presha ya kupoteza ni kubwa kuliko ya kuondoka na ushindi. Unaweza kurudia kutazama Yanga ilivyopata tabu katika dakika za mwisho dhidi ya Geita.
Pili, mashabiki wa Yanga wamepoteza imani na kocha huyo kila wanapoiona timu yao ikiwa haijapata ‘first eleven’ kufikia hatua hii. Manqoba amekuwa muumini wa ‘rotation’ [kubali kikosi], hivyo timu kukosa ‘chemistry’ [maelewano ya kiuchezaji].
Kutokana na sababu mbili hizo, mashabiki wa Yanga wanapata wasiwasi kwamba huenda wakashindwa kutetea ubingwa wa Ligi, achilia mbali kufika hatua ya nusu fainali wanayoiota kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Je, baada ya mapumziko ya sasa ya kalenda ya FIFA, Manqoba atarejea na upepo utakaomuepusha na balaa la kufukuzwa kazi? Na je, atabaki Jangwani hata endapo Yanga itapoteza ‘derby’ yao dhidi ya Simba itakayochezwa Oktoba 10, 2026?


