27.9 C
New York

Mnanda; muziki mzuri uliovaa vazi la uhuni

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazetini

KATIKA miaka ya 1990, muziki wa mnanda, maarufu pia kwa jina la mchiriku, uliwahi kujizolea umaarufu mkubwa hapa nchini, hasa katika Jiji la Dar es Salaam.

Ujumbe na aina ya ala za zilizotumika, mathalan marimba, viliufanya uwe na upekee na uliobea vionjo vya asili vya Tanzania, pengine tofauti na aina zingine za muziki.

Haikuwa Tanzania pekee. Bendi maarufu ya mnanda, Jagwa Cultural Music, iliweza kutanua mbawa zake katika nchi nyingi za ndani na nje ya Bara la Ulaya.

Kipindi hicho mnanda ukawa na nguvu kubwa ya ushawishi kwa wazungu wa mataifa ya Ujerumani, Denmark, Uholanzi, Marekani, Ureno na maeneo mengine duniani.

Ikiwa ni miaka zaidi ya 30 imepita, muziki wa mnanda umepoteza taswira yake si tu nje, bali hata ndani ya nchi, huku wadau wakitaja sababu mbalimbali za anguko la muziki huo.

VAZI LA UHUNI

Fadhili Kimoko ‘Zenden’, chipukizi wa Singeli na mkazi wa Mwananyamala kwa Kopa, Dar es Salaam, ni mpenzi wa mnanda, hasa bendi ya Jagwa, kwa miaka zaidi ya 20, lakini sasa anauona muziki wake huo ukiwa shimoni.

“Sababu kubwa ni uhuni tu. Aina ya watu wanaojifanya mashabiki wa mnanda wamekuwa wakiharibu taswira ya muziki wenyewe. Shoo za muziki wa mnanda zimekuwa zikitawaliwa na matukio mengi ya kihalifu. Wanakwenda kwa lengo la wizi badala ya burudani,” anasema Kimoko.

Mtazamo wake ni kwamba tofauti na Taarabu, Hip hop, R&B na aina zingine za muziki ziliziopo Bongo, shoo za mnanda zinakosa mashabiki wa hadhi na umri tofauti, na badala yake zinabaki na watu wale wale wenye sifa za uhalifu katika jamii.

Katika hilo, Jonas Athanas, prodyuza wa muziki na mkazi wa Bunju, Dar es Salaam, anasema: “Muziki wssenyewe hauna shida na hata ukisikiliza nyimbo zao, utakubaliana na mimi kwamba zimekuwa na ujumbe mzuri mno.

“Shida ni je, kama tunavyoona Bongo Fleva, unaweza kwenda kwenye shoo ya mnanda na ukatarajia kurudi salama bila kuibiwa au kujeruhiwa? Unaweza kuongozana na mzazi, mke au mtoto wako kwenye shoo za mnanda? Hilo ndilo tatizo.

“Leo hii, siku unapochezwa mnanda huku mitaani, majirani wanajificha ndani na wengine kuhama maeneo yao kwa muda, wakihofia kuibiwa au kujeruhiwa.

“Kwamba wanaojifanya wapenzi wa bendi au mnanda, wanatumia shoo kama fursa ya kufanya uhalifu. Muziki hauwezi kuwa hivyo,” anasema Jonas.

Kwa upande wake, Mapunda Silvanus ‘Okocha’, mkazi wa Tabata Relini, Dar es Salaam, anasema kutokana na sura ya uhuni iliyopo kwenye mnanda, imesababisha muziki huo kuzalisha kwa kasi ndogo vipaji vipya.

“Hata kwenye jamii, mtoto anapoingia kwenye uimbaji wa mnanda, tayari anachukuliwa kwa sura tofauti, kwamba ataonekana ameshaharibika. Na ni kweli, hata waimbaji wenyewe, wengi wao kama si walevi, basi ni mateja au wezi.

Lakini, mbali na uhuni, Juma Kiraka ‘Taita’, mkazi wa Mwenge, Dar es Salaam, anasema sababu nyingine ya anguko la mnanda ni kushindwa kwenda sambamba na na mabadiliko ya nyakati. Kivipi?

“Hata kwenye Bongo Fleva, wasanii wengi walioshindwa kwenda na mabadiliko ya kidijitali, hasa matumizi ya mitandao ya kijamii, walianguka.

“Kwa mtazamo wangu, hilo pia lilichangia kwa upande wa mnanda. Viongozi na wanamuziki wenyewe walikosa ‘strategy’ [mkakati] wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia,” amesema.

NINI KIFANYIKE?

Kwa mtazamo wake, Jonas anasema: “Kwanza, wadau wa mnanda wanapaswa kuutenganisha muziki wao na vazi la uhuni na hii inapaswa kuanzia kwenye uongozi wa bendi.

“Waweke mkakati wa kutokomeza matukio ya kihalifu kwenye shoo zao ili kuvutia mashabiki wapya na uwekezaji.

“Mwekezaji hawezi kuweka pesa yake kwenye shoo ambayo kwanza hana uhakika kama itamalizika salama bila matukio ya watu kuibiwa au kuchomwa visu.”

Kiraka, licha ya kushauri bendi za mnanda kwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali, anakiri kuwa vazi la uhuni linapaswa kuvuliwa kwanza, ndipo hatua nyingine zifuate.

“Hata uwe na ‘strategy’ nzuri kiasi gani, haiwezi kuleta matokeo chanya ikiwa bado mashabiki wanahofia kwenda kwenye shoo kwa sababu bado zinatumika kama fursa ya wizi, kujeruhi, kuvuta ‘unga’ au kufanya uhalifu mwingine,” amesema.

Kimoko, kwa upande wake, anazitaka mamlaka kuutupia jicho mnanda, akisema kinaweza kuwa chanzo kingine cha ajira kwa vijana wengi, kama ilivyo kwa Singeli, Hip hop, Taarabu, R&B na aina zingine za muziki.

“Mnanda, kama ilivyo kwa Hip hop na Singeli, ni muziki unaotoka mitaani, ambako vijana wengi hawakutani na fursa nyingi za kiuchumi aidha kwa kuwa wanatokea familia masikini au hawana elimu kubwa,” amesema Kimoko.

Related articles

Recent articles