22.5 C
New York

Tumeisahau jana, tunaiishi leo, tunaitaka kesho!

Published:

Na Hassan Mwasha, Gazeini

KAMA kuna kosa kubwa analoweza kulifanya binadamu katika uso wa dunia ni kujipumbaza kuhusu jana yake. Kusahau kila kitu. Kufuta kumbukumbu nzuri au mbaya juu ya jana yake. Binadamu wa aina hii amepotea!

Binadamu asiye na jana yake hawezi kuiishi leo yenye tija. Anajidanganya! Si kwamba hatoamka asubuhi na kuendelea kupumua, bai hawezi kuiona tija ya leo yake na pia yuko hatarini kuiharibu kesho hata kabla ya kuifikia.

Leo na kesho zilizo bora hujengwa na jana iliyo na msingi imara. Nitakupa mfano uliojengwa kwa swali. Hivi umewahi kujiuliza; ungeianza vipi leo yako endapo ungeamka ukiwa hukumbuki chochote kuhusu jana?

Kwamba kila unapoamka kutoka usingizini, unaanza na kilichopo mbele yako, achilia mbali kukumbuka kama ulilala. Hakuna kumbukumbu ya kwenda kazini, shule au kudai/kudaiwa au kumfuta mtu ambaye mlikubaliana kukutana.

Bila shaka maisha yangekuwa tafrani. Hapo ndipo unapoanzia msingi wa hiyo iitwayo jana, ambayo imebeba siri kubwa katika mfumo wa maisha ya binadamu hapa ulimwenguni. Nitaeleza zaidi.

Katika dunia hii, wapo waliopoteza kila walichofanikiwa kukipata maishani kwa sababu tu ‘walijizima data’ kwa kutokuiheshimu jana yao. Na matokeo yake, leo yao imejaa machungu, ambayo kimsingi yameharibu hata kesho yao.

Nikupe mfano. Hivi karibuni, katika moja ya vipindi vya redio, nilimsikia mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva [sitomtaja jina], ambaye hata hivyo hayupo tena kwenye ‘rotation’ ya soko. Amepotea!

Alisema moja ya mambo anayojutia ni kuwasahau na kuwapuuza watu alioishi nao kabla ya ustaa na waliomsaidia kufika hapo. Kwa ufupi, alikuwa anaijutia jana yake na sasa inamfanya aiishi leo yenye majuto.

Mbaya zaidi, anakumbuka hayo wakati huu akiwa si tena staa na si rahisi tena kurudi pale alipokuwa awali. Hafuatwi na waandishi wa habari, bali yeye ndiye anayetumia nauli yake kuwafuata kwenye vituo vyao vya redio na televisheni akiomba ‘intavyuu’.

Hayuko peke yake katika hilo. Kama binadamu wengine, huenda yumo daktari, muhasibu, mwalimu, kiongozi wa siasa au ‘mtu wa kawaida’ tu huko mitaani, ambaye kwa namna alivyoiishi jana, basi hata leo imekuwa mbaya kwake na haitamani hata kesho yake. Hiyo ndiyo nguvu ya jana.

Uamuzi wako wa jana una nafasi kubwa ya kuumba mateso au furaha unayopitia leo na utakayokutana nayo kesho. Ukifanya utafiti mdogo, asilimia 90 ya matatizo ya leo, msingi wake ni jana.

Kufeli mtihani leo ni matokeo ya mwanafunzi ambaye hakujiandaa jana. Kupata ujauzito usiotarajiwa, Ukimwi au magonjwa ya zinaa ni matokeo ya ngono zembe ya jana. Kuingia ulevini ni matokeo ya marafiki wabaya wa jana.

Kufukuzwa kazi leo ni matokeo ya uvivu wa jana ofisini. Hata asilimia 99 ya vifo vya kujiua hutokana na maumivu ya kilichotokea jana. Ni ngumu leo ikazalisha kitendo na matokeo kwa wakati mmoja.

Hivyo basi, ni busara kuitanguliza jana katika kila hatua ya kuiendea leo, kabla ya kuifikia kesho yako. Lakini je, ipi bora kuanza nayo kati ya jana ya leo au jana ya kesho? Zote ni jana na zote zina uzito unaolingana. Tafakari!

Related articles

Recent articles