LA PAZ, Bolivia
WATU wawili wamepoteza maisha katika mlipuko uliotokea katika kambi ya jeshi nchini Bolivia, ingawa mamlaka zinadai kuwa huenda idadi ya vifo ni kubwa zaidi.
Aliyethibitisha kutokea kwa mlipuko huo ni Waziri wa Ulinzi wa Bolivia, Ernesto Justiniano, akisema watu 81 wamejeruhiwa na wengine saba hawajulikani walipo.
Katika taarifa nyingine tofauti iliyotolewa na Wizara ya Afya, watu 10 hadi 15 walipoteza maisha kwenye mlipuko huo ulitokea mjini Viacha.
Aidha, polisi wameeleza kuwa nyumba zaidi ya 10 za raia zimeharibiwa na mlipuko huo. Madai ya kutokea kwa mlipuko nayo yameripotiwa.
Kwa hofu hiyo, raia wanaoishi karibu na kambi za jeshi wametakiwa kuhama, walau kuwa nazo kwa umbali wa mita 150.
Wakati huo huo, Rais wa Bolivia, Rodrigo Paz, ameeleza kusikitishwa na taarifa hizo, akisema mamlaka ziko pamoja na familia za waliofariki na waliojeruhiwa.


