TUNIS, Tunisia
MAHAKAMA nchini Tunisia imetoa agizo la kukamatwa na kushikiliwa kwa mwandishi wa habari maarufu, Mohamed Yousfi, jana Septemba 4, 2026.
Aidha, mahakama ilieleza kuwa Yousfi anakabiliwa na mashitaka mbalimbali, yakiwamo ya utakatishaji wa fedha.
Katika kutii agizo, polisi wamemkamata Yousfi wakati mwandishi huyo alipowasili kwa mahojiano kwenye kituo cha redio cha Radio Express FM.
Aliyetoa taarifa za kukamatwa kwake ni Rais wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Tunisia [SNJT], Zied Dabbar.
Aidha, Dabbar, kwa upande wake, ameeleza kuwa kukamatwa kwa mwandishi huyo ni matokeo ya ukosoaji anaofanya dhidi ya serikali.
Yousfi, ambaye ni mhariri mkuu wa tovuti ya habari za uchunguzi ya Al-Qatiba, amekuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa Rais Kais Saied.
Akiendelea kumzungumzia Yousfi, SNJT imeeleza kuwa kushikiliwa kwa Yousfi ni mwendelezo wa uminyaji wa uhuru wa kujieleza.
Mbali na waandishi, pia wanasheria, wanasiasa wa upinzani na wanaharakati wamekuwa wakifunguliwa kesi nchini Tunisia.


