BUENOS AIRES, Argentina
‘NIMETOA kila kitu, sina nilichobakiza.’ Ni kauli ya Lionel Messi wakati alipotangaza hivi karibuni, kwamba amestaafu kuitumikia timu ya soka ya Taifa ya Argentina.
Ni kweli hana alichobakiza. Messi (39), amestaafu akiwa ndiye mfungaji bora wa muda wote (mabao 125) wa Argentina. Wakati huo huo, ndiye mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi (207) katika historia ya timu hiyo.
Kama hiyo haitoshi, ameipa timu hiyo mataji yote makubwa, tena akiwa ndiye nahodha wa kikosi. Aliiongoza Argentina kutwaa taji la Copa America mara mbili (2021 na 2024) na Kombe la Dunia (2022).
Hii si mara ya kwanza kustaafu. Alifanya hivyo mwaka 2016 lakini tangu arejee uwanjani kutokana na ushawishi wa benchi la ufundi na Rais wa Argentina, Mauricio Macri, Messi amefunga mabao 70 katika mechi 94.
Safari hii, anaondoka akiwa amefunga ule mjadala maarufu wa nani shujaa wa Argentina kati yake na Diego Maradona. Miaka 10 iliyopita, wengi walisema Messi hajamfikia Maradona kwa sababu hana Kombe la Dunia. Alizima hoja hiyo mwaka 2022 nchini Qatar.
Maradona, kwa upande mwingine, anaachwa mbali na Messi linapokuja suala la mafanikio ya ngazi ya klabu. Messi tayari ana mataji nane ya La Liga na manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Tangu kifo cha baba yake, Jorge, zilikuwapo hisia kwamba huenda safari ya Messi katika mchezo wa soka isiwe ndefu.


