WASHINGTON DC, Marekani
IKIWA ni miezi sita imepita tangu vilipoanza vita kati ya Iran na Marekani inayoshirikiana na Israel, mambo yamezidi kuwa magumu kwa pande mbili hizo kufikia mwafaka wa kuweka silaha chini.
Iran, ambayo ilionekana ingeshindwa mapema, imeendelea kuivimbia Marekani, huku hatima ya Mlango-Bahari wa Hormuz ikiendelea kuwa kitendawili.
Marekani, kwa kuona mambo yamekuwa magumu, hivi karibuni ilitangaza vikwazo vipya vya kiuchumi kwa Iran, pia ikizionya nchi, taasisi na mashirika yanayofanya biashara na Taifa hilo la Kiarabu.
Je, ni yapi yaliyoonekana kuchomoza tangu vita hivyo vilipoanza rasmi Februari 28, 2026, ambapo Marekani na Israel ndizo zilizoanza kuishambulia Iran? Makala haya yanachambua.
TRUMP KICHWA KINAUMA
Tangu kuanza kwa vita, ushawishi wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ndani na nchi hiyo umeshuka kutoka asilimia 40 hadi asilimia 33, kwa mujibu wa utafiti wa taasisi ya Ipsos.
Gharama ya gesi imepanda, tofauti na ahadi aliyotoa wakati wa kampeni za urais za mwaka 2024, kwamba ingeshuka na kuwa nafuu zaidi kwa raia wa Marekani.
Pia, tofauti na ahadi yake ya kuindosha Marekani katika migogoro, wananchi wanaiona nchi yao ikiwa kwenye hali mbaya zaidi, hasa kipindi hiki cha vita dhidi ya Iran.
Takwimu zinaonesha kuwa ni asilimia 31 tu ya raia wa Marekani wanaounga mkono vita hivyo. Ni idadi ndogo zaidi, ukilinganisha na waliokuwa wakikubaliana na vita dhidi ya Afghanistan.
Vita hivyo dhidi ya Iran pia vimesababisha mpasuko ndani ya Chama chake cha Republican, ambapo baadhi ya wanasiasa hawaoni umuhimu wa nchi yao kuendelea kupigana na Iran.
MTIKISIKO WA KIUCHUMI
Asilimia 20 ya mafuta na gesi asilia zinazoingia kwenye soko la dunia husafirishwa kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz. Kwa miaka mingi, Iran imekuwa ikiidhibiti njia hiyo ya maji.
Kutokana na vita, Iran imeongeza udhibiti na wakati mwingine kufunga Hormuz, hivyo kuathiri upatikanaji na kusababisha kupanda kwa bei ya nishati hizo.
Ni kutokana na changamoto hiyo, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) linabashiri kuwa uchumi wa dunia utapanda kwa asilimia 3 tu mwaka 2026, tofauti na asilimia 3.3 iliyotarajwa hapo awali.
IRAN IMETHIBITISHA UIMARA WAKE
Mei, 2026, kamanda mkuu wa Marekani huko Mashariki ya Kati, Brad Cooper, alijinasibu kuwa vikosi vyake vimeshambulia meli 161 za Iran na kuharibu asilimia 82 ya mifumo yake ya anga.
Licha ya hasara hizo, Iran haijarudi nyuma, na badala yake imeendelea kutekeleza mashambulizi dhidi ya Marekani na washirika wake walioko Mashariki ya Kati, ikiwamo Saudi Arabia.
Bado jeshi la Iran limeendelea kutumia ndege zake zisizo na rubani (drones) kushambulia meli na hata kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Mashariki ya Kati.
SILAHA ZA NYUKLIA
Pigo kubwa walilopata Iran katika vita hivyo ni kushambuliwa na kusambaratishwa kwa vinu vyake vitatu vya utengenezaji wa silaha za nyuklia. Hilo lilifanyika Juni, 2025.
Taarifa zinaeleza kwamba pia mashambulizi mazito yaliyofanywa na Israel nchini Iran yalisababisha vifo vya wanasayansi wa nyuklia waliokuwa kwenye vinu hivyo.
Ni kwa maana hiyo basi, wachambuzi wa masuala ya usalama wanaamini kuwa huenda ikaichukua muda mrefu Iran kurejesha mfumo wake mzima wa utengenezaji wa silaha za nyuklia.
UBABE WA MAREKANI UMEKWISHA?
Kupitia vita hivyo, Iran imeithibitishia dunia kuwa Marekani si ya kuhofiwa tena. Katika vita hivyo, wanajeshi wake 18 wameuawa na wengine zaidi ya 750 kujeruhiwa.
Pia, jeshi la Marekani limepoteza ndege zake za kijeshi na zisizo na rubani. Katika utafiti uliofanyika Mei, 2026, ilielezwa kuwa ndege zilizopotezwa na Iran ni takribani 42.


