23.5 C
New York

Mwandishi aliyemfuata mafichoni Osama bin Laden (3)

Published:

Na mwandishi wetu, Gazetini

KATIKA sehemu ya pili ya makala haya, tuliona Osama akihojiwa na Miller akieleza chanzo cha uhusiano wake mbaya na Marekani, ambapo alisema mambo mawili.

Mosi, aliishutumu Marekani kwa namna inavyowachukulia vijana wa Palestina magaidi, wakati wao ndiyo wakubwa zaidi kwenye shughuli hiyo. Pili, alisema aliichukua Marekani kwa namna ilivyoiwekea vikwazo Iraq na kusababisha vifo vingi vya watoto. Tuendelee …

Februari 26, 1993, tukio la kushambuliwa kwa bomu Kituo cha Biashara cha Kimataifa jijini New York kiliibua taharuki kubwa nchini Marekani. Watu sita walifariki na maelfu kujeruhiwa.

Linatajwa kuwa shambulizi la kwanza la kigaidi la kimataifa kutekelezwa katika ardhi ya Marekani. Aliyetega bomu hilo alitajwa kwa jina la Ramzi Yousef, ambaye hata hivyo alifanikiwa kutoroka saa chache tu baada ya tukio.

Baada ya miezi mingi iliyohusisha kukamatwa kwa Waislam wengi wakihusishwa na shambulizi hilo, Shirika la Ujasusi lilijiridhisha kuwa Yousef alikuwa sehemu ya wapiganaji wa moja ya vikundi vilivyo chini ya Osama.

Miezi michache baadaye, Yousef alionekana Manila, Ufilipino, akiwa na mmoja ya watu wa karibu wa Osama, Wali Khan Amin Shah. Kukutana kwao kulihusishwa na mipango ya kuendeleza moto dhidi ya Wamarekani na washirika wao.

Hatimaye, Yousef alitiwa mkono na FBI mwanzoni mwa mwaka 1995 akiwa nchini Pakistan. Alikutwa akiishi kwenye moja ya nyumba za wageni mjini Islamabad, ambayo inaelezwa kuwa wapiganaji wengi wa Osama waliitumia kwa makazi.

Miller alipomuuliza Osama juu ya tukio hilo na uhusiano wake na Yousef, alikana kumjua akisema: “Kwa bahati mbaya, nimemjua baada ya tukio.”

Khan, kwa wasiomfahamu, aliwahi kukiri kuwa Osama alimtuma wakati fulani mjini Ufilipino kwa ajili ya kufuatilia njia ambazo Rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton, angezitumia katika ziara yake nchini humo ili watege bomu la kumuua.

Je, ni kweli Osama aliwahi kusuka mpango wa kumuua Clinton? Ni swali jingine la Miller alilomsukumia katika mahojiano yao mjini Islamabad mwaka 1998.

“Kama nilivyosema, kila kitendo hupata mrejesho unaendana nacho. Clinton anategemea nini kutoka kwa wale aliowaua, kutesa watoto na mama zao?” alihoji Osama kuthibitisha mpango wao huo.

Osama alisisitiza kuwa ugaidi ndiyo njia pekee ya kuipa presha Marekani iache uonevu na chuki si tu dhidi ya Palestina, bali mataifa ya Kiislam, na kuacha kuiunga mkono Israel.

“Hivyo, tunataka kuwaambia mama wa wanajeshi kwamba kama wanajali maisha yao na ya watoto wao, basi wachague serikali ambayo itaangalia masilahi yao na si kulinda Wayahudi,” alisema Osama.

NB: Hii ni sehemu ya mwisho ya mfululizo wa makala haya ya ‘Mwandishi aliyemfuata mafichoni Osama bin Laden’ … Kama ulipitwa na sehemu zilizopita, tembelea www.gazetini.co.tz.

Related articles

Recent articles